Kwa kutambua umuhimu wa wakulima wakati wa utekelezaji wa miradi ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia inayotekelezwa nchini, Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imekita kambi Jijini Dodoma kushiriki Maonesho ya Nane Nane mwaka 2024 kueleza nafasi ya wakulima katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Sanjari na hilo, PURA pia inaeleza fursa zilizopo kwa wakulima wakati wa utekelezaji wa miradi ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia na namna ambavyo sekta ya kilimo na sekta ya mafuta na gesi asilia zinategemeana.
“Miradi yote inayotekelezwa ikiwemo miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia inahusisha mkusanyiko wa idadi kubwa ya watu, ikiwemo wafanyakazi na vibarua katika maeneo inakotekelezwa miradi hiyo, ambao hutegemea chakula kinachotokana na mkulima. Bila ya mkulima, ni dhahiri kuwa utekelezaji wa miradi utaathirika. Hivyo, kwetu sisi, mkulima ni mdau muhimu na ndio maana tunashiriki maonesho haya” alieleza Bw. Ebeneza Mollel kutoka PURA.
Bw. Mollel alieleza pia kuwa, mbali na wakulima kuwa chanzo cha chakula kwa watu wanaofanya kazi katika miradi ya mafuta na gesi asilia, gesi asilia inayozalishwa nchini inaweza kutumika kuzalisha mbolea hivyo kunufaisha wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla.
“Ingawa kiwanda cha kuzalisha mbolea kwa kutumia gesi asilia bado hakijajengwa nchini, Serikali kupitia mamlaka zake imeendelea kuweka juhudi kuhakikisha viwanda hivyo vinajengwa” aliendelea Mollel.
PURA, kama mdhibiti na mshauri wa masuala ya mkondo wa juu wa petroli, ina jukumu la kuhakikisha, pamoja na mambo mengine, uhakika wa upatikanaji gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa mbolea.