Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amezitaka Hospitali zote na vituo vya Afya nchini kuhudumia wagonjwa wa nje wanaofika kupata huduma kwa masaa yasiyozidi matatu.
Waziri Jenista amesema hayo leo Agosti 20, 2024 wakati alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General) ili kuona hali ya utoaji wa huduma sambamba na kuongea na watumishi waliopo Hospitalini hapo.
Amezitaka Hospitali zote nchini na kuziagiza kuzingatia mzunguko wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa na kuhakikisha mzunguko huo unatumia masaa ya kitaalamu ambayo hayazidi masaa matatu kwa kila mgonjwa na kupunguza muda wa wagonjwa kukaa hospitali kusubiri huduma.
“Mgonjwa anapofika katika kituo cha afya au Hospitali asianze kuwaza ameenda kukaa sehemu hiyo kwa siku nzima na hivyo kusitisha shughuli zake nyingine, zingatieni mzunguko mzima wa utoaji huduma kwa wagonjwa kwa kuzingatia muda wa utaalam usiozidi masaa matatu”. Amesema Waziri Mhagama.
Ameongeza kuwa muda huo ni kuanzia mgonjwa anapofika hospitalini kwa kuanza kujiandikisha, kumuona daktari, wakati anapatiwa matibabu na kupatiwa dawa kwamba mzunguko huo wa mgonjwa usizidi masaa matatu.
Ili kufanikisha hilo Waziri Mhagama amesisitiza uwepo wa matumizi ya TEHAMA pamoja mifumo kusomana ikiwa njia ndiyo njia pekee ya kuokoa muda na kutoa huduma bora kwa mgonjwa ikiwa ni sehemu ya kupunguza malalamiko ya mara kwa mara.
“Matumizi ya Tehama yatasaidia na kurahisisha mifumo ya matibabu na taarifa za mgonjwa kufanana na pia hata kurahisisha huduma kwa mgonjwa wakati atakapokuwa yupo hospitalini anatibiwa”. Amesema Waziri Mhagama.
Kwa upande mwingine, Waziri Mhagama wamewataka watumishi wa afya kuwa na lugha ya staha wanapohudumia mgonjwa kwani lugha nzuri ni kichocheo kimojawapo cha kumpa ahueni mgonjwa na kujisikia vizuri.
Halikadhalika, amewahakikishia watumishi wa afya nchini kushirikiana nao ili kuweza kuhakikisha huduma bora za afya zinaendelea kutolewa kwa wananchi na mtumishi yeyote mwenye shida ya kumuona milango iko wazi.