Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameupongeza uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa mipango madhubuti ya kuboresha na kujenga miundombinu mipya kwa lengo la kupanua na kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi; katika kufungamanisha mahitaji ya miundombinu na ongezeko la wanafunzi wanaomaliza elimu ya sekondari.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo leo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi awamu ya kwanza Kampasi ya Babati mkoani Manyara, ambayo inajumuisha ujenzi wa jengo la taaluma litakalochukua zaidi ya watu 2600 , hosteli zenye uwezo wa kuchukua watu 1456 na bwalo la chakula; ambao utagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.
“IAA mnafanya vizuri na mnatupa heshima wote; hakuna kitu kinamuudhi Mhe. Rais kama apambane fedha zipatikane ili huduma ziwafikie wananchi halafu huduma zile zisiwafikie wananchi, lakini ninyi mnavyosimamia vizuri fedha na kazi inaonekana mnatutengenezea heshima wote, hongereni sana, amesema,” Dkt. Mwigulu.
Ameongeza kuwa serikali inatambua jitihada za uboreshaji miundombinu ya kujifunzia na kufundishia zinazofanyika katika kampasi za Arusha, Dodoma na Babati na inatambua mchango wa IAA katika kuandaa wataalam wenye ujuzi wa wa hali ya juu katika fani za uhasibu, fedha, uchumi, TEHAMA na nyingine nyingi.
Mkuu wa Chuo IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema baada ya kukamilika kwa jengo la taaluma lenye ghorofa tano litakalokuwa na ofisi, madarasa, kumbi za mihadhara, maabara za kompyuta, chuo kupitia mradi wa HEET kitajenga jengo la maktaba na Kituo cha TEHAMA; awamu ya tatu IAA ikitarajia kujenga viwanda nane vya kufundishia, mabweni na viwanja vya michezo.
Aidha, Prof. Sedoyeka amesema IAA ni Kampasi ya kimkakati hivyo IAA inatarajia kuandaa mitaala inayoendana na uhalisia, mahitaji ya soko na mategemeo ya watu wa Manyara, ambapo amebainisha kuwa mitaala hiyo italenga maeneo ya mifugo, kilimo, madini ambazo ni shughuli za kkiuchumi za watu wa Manyara.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga amesema uwepo wa Kampasi ya Babati ya IAA mkoani humo utawasaidia wananchi kupata elimu bora na kuinua uchumi wao kupitia uwekezaji katika huduma mbalimbali zitakazohitajika na wanafunzi.
Kampasi ya Babati ilianzishwa mwaka 2014 na imepata ithibati kamili Julai 2024, hivyo imeongeza wigo wa udahili katika fani za Uhasibu, Usimamizi wa biashara, TEHAMA, Ununuzi na Ugavi, Fedha na Benki, Sayansi ya Kompyuta, Uhasibu na Tehama, Usimamizi wa Rasilimali watu na Mifumo ya Mawasiliano ya Kompyuta.