Waziri wa Maliasili na Utalii Angelah Kairuki amewataka watanzania kujijengea utamaduni wa kutembelea vivutio mbalimbali ili kufahamu asili yao na urithi wao ambao umerithishwa kwa jamii.
Waziri Kairuki ametoa kauli hiyo wakati wakati akitembelea mabanda mbalimbali taasisi zilizochini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwemo Bodi ya Utalii TTB katika maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa maarufu kama sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya mwalimu nyerere jijini Dar es salaam.
Waziri Kairuki amesema kuwa ni vyema jamii ikatumia fursa ya uwepo wa maonyesho hayo kujifunza na kujionea masuala mbalimbali ya utalii ili kujiongezea utamaduni wa kujua historia ya nchi yao.
‘Ni umuhimu kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na mwingiliano wa Taasisi za Serikali zilizopo na makampuni binafsi yanayoshiriki kwenye Maonesho hayo kwa lengo la kukuza mahusiano yatakayoleta tija’amesema Waziri Kairuki
Aidha Waziri Kairuki ametoa rai kwa Wazazi wenye wanafunzi waliohitimu kidato cha nne kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii na kuzungumza na wataalamu katika vyuo vilivyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kama Chuo cha Misitu Olmotonyi, Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI), Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA), Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) na vyuo vingine ili kujua fursa mbalimbali za kujiunga na vyuo hivyo.
Chance Ezekiel ni Afisa Utamaduni kutoka Makumbusho ya Taifa la Tanzania amemueleza Waziri Kairuki baada ya kutembelea banda lao kuwa lengo la makumbusho hiyo ni kuhakikisha wanawajulisha watanzania umuhimu wa kuenzi na kupenda urithi wao.
Ili kuendeleza masuala ya teknolojia Waziri Kairuki amesema kwa mwaka huu wamekuja na mfumo VR (Virtual Reality) ambayo inaonyesha matendo ya moja kwa moja kwa wakati huo katika hifadhi mbalimbali.