Home LOCAL TMDA YAKANUSHA UWEPO PARACETAMOL INAYOBABUA NGOZI

TMDA YAKANUSHA UWEPO PARACETAMOL INAYOBABUA NGOZI

Na:  Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekanusha uwepo wa Dawa ya Paracetamol inayodaiwa kubabua ngozi.

Kwa mujibu wa taarifa liyotolewa kwa umma na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, imesema taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa dawa hiyo, haina ukweli na kuwataka wananchi waipuuzie.

Akinukuu taarifa hiyo inayosambazwa mitandaoni:

“Dawa hiyo inadaiwa kuwa ni ‘’paracetamol mpya nyeupe sana na inayong’aa, madaktari wanashauri kuwa ina virusi vya “Machupo”, inayochukuliwa kuwa moja ya virusi hatari zaidi ulimwenguni, na kiwango cha juu cha vifo.

Aidha, mtoa taarifa anaitaka jamii kuisambaza taarifa hiyo kwa kila mtu aliyeko katika orodha yake ya mawasiliano ili kuokoa maisha.

Anamalizia kwa kusema ‘’Nimefanya
sehemu yangu, sasa ni zamu yako. Kumbuka kwamba Mungu huwasaidia wale wanaosaidia wengine. ‘’Sambaza kama ilivyopokelewa’’.

Dkt.Fimbo ameeleza kuwa, taarifa hiyo imekuwa ikijirudia mara kwa mara na TMDA imekuwa ikitolea ufafanuzi ikiwemo taarifa ya mnamo tarehe 10 Mei, 2023, juu ya dawa aina ya P-500® (PARACETAMOL) ya Apex Laboratories Private Limited, Tamil Nadu, India
iliyodaiwa kuwa na virusi hivyo.

“TMDA inapenda kuufahamisha umma kwa mara nyingine kwamba hakuna virusi vinavyojulikana kwa jina la Machupo. Aidha, virusi vya aina yoyote haviwezi kuishi kwenye kidonge.

Dawa zenye kiambata hai cha paracetamol inayotumika kutibu homa na maumivu zilizopo katika soko nchini kwa majina mbalimbali ya kibiashara zimesajiliwa baada ya kuthibitishwa kuwa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi unaotakiwa na hivyo, ni salama kwa matumizi yaliyoainishwa,” ameongeza.

Katika hatua hiyo, TMDA inapenda kuwahakishia wananchi kuwa inaendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda afya ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa bidhaa tiba zinazotumika nchini ni zile zenye kukidhi matakwa ya ubora, usalama na ufanisi.

Vilevile, mamlaka inapenda kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kupata ufafanuzi kutoka kwenye mamlaka husika kabla ya kusambaza taarifa zinazoweza kuleta taharuki kwenye Jamii.

TMDA ndio yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa tiba nchini ambapo ili kuhakikisha kuwa bidhaa tiba (zikiwemo dawa) zilizoko katika soko nchini zinakidhi matakwa ya usalama, ubora na ufanisi, TMDA imeweka mifumo mbalimbali ya udhibiti ikiwa ni pamoja na tathmini na usajili, ukaguzi, uchunguzi wa kimaabara na ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa katika soko.

Aidha, amesema wananchi wanaweza kupiga simu ya bila malipo: 0800110084 endapo wapatapo taarifa za mashaka kama hizo.

Mwisho.

Previous articleKATIBU MKUU DKT NCHIMBI AZURU KABURI LA HAYATI MKAPA, CCM YATOA MILIONI 10 KUENDELEZA MAJENGO YA SHULE LUPASO
Next articleKAMPUNI YA SWALA SOLUTION YAWAJENGEA NYUMBA WALIMU MSALALA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here