Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye viwanja vya Ikulu kwa ajili ya kuzungumza na Machifu kutoka Mikoa mbalimbali nchini, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Julai, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Akiwa kwenye picha ya pamoja na Machifu kutoka Mikoa mbalimbali nchini katika viwanja vya Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Julai, 2024.
DODOMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameilekeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kukamilisha Mwongozo wa Utambuzi wa Machifu na Viongozi wa Kimila katika Wilaya na Mikoa utakaoainisha majukumu yao wa kimila na kijadi.
Rais Dkt. Samia ametoa maelekezo hayo leo wakati akizungumza na Viongozi wa Kimila na Machifu kutoka Tanzania nzima kwenye hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino.Ā
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema Viongozi wa Kimila na Machifu wana mchango mkubwa katika kulinda maadili na kutatua changamoto za kimaadili katika jamii licha ya kuwa yanashughulikiwa katika ngazi ya Serikali.
Rais Dkt. Samia pia ametoa rai kwa Machifu kote nchini kuendelea kujenga mvuto na uaminifu wa watu ili waweze kutoa mchango wao ipasavyo kwa ushrikiano na Serikali katika utatuzi wa migogoro inayoikabili jamii.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amekemea vitendo vya utekaji na mauaji ya watoto kwa imani potofu za ushirikina ambayo ni kinyume cha maadili ya Watanzania na kuwasihi Machifu na wananchi woteĀ kukemeaĀ vitendo hivyo.Ā Ā
Vilevile, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara hiyo kuimarisha michezo ya Umoja wa Michezo ya Shule za Msingi na Sekondari (UMISSETA na UMITASHUMTA) ikiwa ni sehemu ya kuwafundisha na kudumisha mila na desturi zetu.
Rais Dkt. Samia pia amesema dunia inaposhuhudia mabadiliko mbalimbali, Serikali ya Tanzania itahakikisha kuwa inashuhudia maendeleo ambayo yanadumisha mila na desturi za Watanzania.
Sharifa B. Nyanga
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu