Home BUSINESS NHC YATEKELEZA MRADI WA SAMIA HOUSING SCHEME KWA MAFANIKIO MAKUBWA

NHC YATEKELEZA MRADI WA SAMIA HOUSING SCHEME KWA MAFANIKIO MAKUBWA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Ahmed Abdallah Ahmed akizungumza alipokuwa akiwasilisha taarifa ya miradi mitatu inayotekelezwa na Shirika hilo, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, wakati wa ziara ya kukagua miradi mitatu ya NHC  Juni 30,2024, Jijini Dar es Salaam .

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Ahmed Abdallah Ahmed (kulia), akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Tomotheo Mzava, (katikati), na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda, (wa pili kushoto), wakikagua Mradi wa Kawe711, wakati wa ziara ya Kamati hiyo.

DAR ES SALAAM 

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea na uwekezaji wa ujenzi wa nyumba 5000 za gharama nafuu na kati, katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara kupitia mradi wa Samia Housing Scheme iikiwa ni uwekezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza miradi ya Shirika hilo iliyokuwa imesimama kwa muda mrefu.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Ahmed Abdallah Ahmed alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi mitatu ya NHC kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipofanya ziara ya kukagua miradi hiyo Juni 30,2024 Jijini Dar es Salaam.

Ahmed amesema kuwa asilimia 50 ya mradi huo utatekelezwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo asilimia 20 ya nyumba nyingine zitajengwa Dodoma na 30 katika mikoa mingine.

“Mradi huu wa SHS ni mradi wa nyumba za kuuza na kupangisha, na unakusudia kuenzi kazi nzuri anayofanya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa nyumba bora hapa nchini” amesema Ahmed.

Aidha ameongeza kuwa mradi huo utatekelezwa kwa awamu, na kwamba utagharimu kiasi cha Sh.Bilioni 466 sawa na Dola za Marekani Milioni 200.

“katika kuendeleza mradi huu, Nyumba 560 zinaendelea kujengwa katika eneo la Kawe ambapo hadi kufikia leo Juni 30, 2024 ujenzi wake umefikia asilimia 65. 

“Mradi huu wa Kawe utagharimu kiasi cha Sh.Bilioni 48.27 na hadi sasa takribani kiasi cha Sh.Biliioni 21.88 zimeshatumika,” ameongeza Ahmad.

Pia amesema kuwa hadi sasa mauzo ya mradi huo yamefikia asilimia 100 na tayari Shirika limepokea malipo ya awali ya kiasi cha Sh.Bilioni 31.2 ambapo kiasi kilichobaki cha Sh.Bilioni 45.5 kinaendelea kukusanywa.

Kuhusu Mradi wa Morocco Square, Ahmad amesema kuwa umekamilika kwa asilimia 99 na shughuli za upangishaji tayari umeanza kwa baadhi ya maeneo ikiwemo hoteli yenye vyumba 81, na eneo la Ofisi za Biashara upangishaji unaendelea kukamilika.

Aidha amesema jengo lenye nyumba za makazi 100, tayari zimekamilika na kwamba nyumba 71 zimeshauzwa, na nyumba zilizobaki zinaendelea kuuzwa.

Aidha katika mradi huo tayari Shirika limekusanya kiasi cha Sh.Bilioni 30, na kiasi cha Sh.Bilioni 35.9 kinaendelea kukusanywa huku eneo la maduka limeshapangishwa kwa asilimia 98 ambapo kwasasa upangaji wa bidhaa unaendelea ili kufungua maduka hayo mwezi Julai mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here