Kaimu Meneja wa kiwanda cha kuzalisha mpira ya mikono (Groves), cha MSD kilichopo Idofi, Makambako mkoani Njombe Bw. Shiwa Mushi akitoa maelezo kwa wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea kiwanda hicho Julia 2,2024 Mkoani Njombe.
Afisa Uhusiano Mkuu wa MSD, Etty Kusiluka akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kukamilika kwa ziara ya wahariri wa vyombo vya habari Mkoani Njombe.
NJOMBE
Uzalishaji wa Bidhaa za mipira ya mikono (Gloves), katika kiwanda kinachomilikiwa na Bohari ya Dawa (MSD), kilichopo Idofi, Makambako mkoani Njombe, umefikia zaidi ya jozi milioni mbili toka kilipoanza uzalishaji wa Bidhaa hiyo mwezi Februari Mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa kiwanda hicho, Shiwa Mushi, alipozungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari waliotembelea kiwandani hapo Julai 2,2024 kujifunza na kujionea namna kinavyofanya kazi.
Katika wasilisho lake Mushi ameeleza kuwa Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha Jozi Milioni 86.4 sawa na asilimia 83.4 ya mahitaji ya nchi kwa mwaka.
Amesema Kiwanda hicho kinamilikiwa na (MSD) kupitia kampuni yake tanzu ya Medipham Manufacturing CO LTD, na kwamba kina uwezo wa kuzalisha jozi 10,000 kwa wiki.
Aidha ameongeza kuwa Kiwanda hicho ujenzi wake ulianza rasmi mwaka 2020, ambapo ulitokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona ulioibuka Tanzania na Dunia kwa ujumla.
Ameongeza kuwa mbali na Kampuni hiyo tanzu kumiliki kiwanda hicho, pia inamiliki viwanda vingine viwili ambavyo vipo katika hatua za mwisho.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano Mkuu wa MSD, Etty Kusiruka, amesema kuwa awali kabla ya kuanzishwa kiwanda hicho, Taasisi hiyo ilikuwa ikinunua bidhaa hiyo na kuisambaza kwa wadau, ikiwemo Hosptali, vituo vya Afya na Zanahati.
“Uwepo wa kiwanda hiki unasaidia zaidi ya asilimia 80 ya kuagizwa bidhaa hii nje ya nchi, na kuokoa fedha za Serikali. kabla ya kuanzishwa kwa kiwanda hiki MSD ilikuwa mdau mkubwa wa kununua bidhaa hizi, kuuza na kuzisamba kwa wadau, ikiwemo Hosptali , Vituo vya Afya na zanahati” amesema