Home LOCAL KAMPENI UCHAGUZI TLS ZAPAMBA MOTO

KAMPENI UCHAGUZI TLS ZAPAMBA MOTO

Picha zikiwaonyesha wagombea Mbalimbali wanaowania nafasi ya Chama Cha Wanasheria Tanzania (TLS)

Na Mwandishi Wetu

WAGOMBEA wa nafasi ya urais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), jana wameshiriki mdahalo wa kunadi sera zao huku wengi wakiwa na shauku ya kuimarisha heshima ya mawakili nchini.

Agosti mosi hadi 3, mwaka huu, chama hicho kinatarajia kufanya mkutano mkuu wake ambao moja ya majukumu ni kumchagua Rais wa TLS.

Wagombea wanaowania nafasi hiyo ni Wakili Sweetbert Nkuba, Paul Kaunda, Revocatus Kuuli, Emmanuel Muga, Ibrahim Bendera na Boniface Mwabukusi.

Katika mdahalo huo ulioandaliwa na moja ya chombo cha habari cha televisheni nchini, wagombea hao wamenadi sera zao ambapo Mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, Sweetbert Nkuba, alisema anauzoefu wa muda mrefu wa uongozi katika ngazi mbalimbali na kuomba achaguliwe kwenye nafasi hiyo ili afanikishe vipaumbele vitano ikiwemo kuwaunganisha wanachama wa TLS na kuhakikisha maslahi ya kiuchumi ya wanachama wa chama hicho yanazingatiwa.

Alisema atahakikisha inatungwa sera ya jinsia kwa TLS na atalinda na kuitetea taaluma ya uwakili kwa wivu mkubwa.

Wakili Nkuba alisema anaamini uimarishaji wa miundombinu ya kisheria na kiteknolojia ndani ya TLS utawezesha huduma bora kwa wanachama na jamii kwa ujumla kwa kuongeza uwekezaji katika mifumo ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma za kisheria.

Pia alisema akichaguliwa atazingatia masuala ya mafunzo na utaalamu ili kuhakikisha kuwa wanasheria wana ujuzi wa kisasa na uwezo wa kushindana kimataifa.

Alisema sera yake ni ushawishi na utetezi kwa kuhakikisha TLS inakuwa na sauti yenye nguvu katika masuala ya kitaifa na kimataifa yanayohusu sheria na haki.

“ Hii itajumuisha:Kuanzisha mikakati ya ushawishi kwa serikali na bunge ili kuboresha mfumo wa sheria nchini, kutoa msaada wa kisheria kwa jamii, hususan makundi yenye uhitaji maalum,”alisema.

Kadhalika, alisema atazingatia uwajibikaji kwa kusimamia kwa uwazi na uwajibikaji katika shughuli zote za TLS ili kujenga imani kwa wanachama na wadau wengine ikiwamo kuboresha mifumo ya ukaguzi wa ndani na nje ili kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali za TLS na kuanzisha utaratibu wa kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wanachama kuhusu shughuli na matumizi ya fedha za TLS.

“Nimedhamiria kujenga mahusiano imara kwa wadau mbalimbali, ikiwamo serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na taasisi za kimataifa. Hii itajumuisha: Kuanzisha na kudumisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa ya kisheria kwa manufaa ya wanachama wa TLS, Kushirikiana na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu katika kutoa elimu ya sheria na mafunzo ya vitendo,”alisema.

Kadhalika, alisema atakuza uongozi na ushirikishwaji kwa kuhakikisha wanachama wa TLS wanashiriki kikamilifu katika maamuzi na uongozi wa chama.

“Nitaanzisha mfuko wa malipo ya ada yam waka kwa unafuu, kuanzisha na kusimamia vituo vya malezi kwa mawakili wapya, upatikanaji wa bima ya afya kwa utaratibu wa kulipa kidogo kidogo,”alisema.

Naye, Mgombea Wakili Paul Kaunda alisema anataka kuwalinda na kuwatetea mawakili wachanga kwa kuwaongezea thamani na heshima ikiwamo kuja na Wakili APP ambayo itasaidia mawakili kupata wateja kwa urahisi na kupata malipo stahiki kwa mujibu wa sheria ya gharama za mawakili itakuwa kama UBA.

Alisema atamshauri na kumshirikisha mwanasheria mkuu wa serikali kutunga kanuni zitakazotulinda mawakili na kuwaheshimisha mawakili wanapofanya majukumu wao wakiwa Mahakamani, polisi na vyombo vingine.

Pia alisema atamshauri na kumshirikisha Jaji Mkuu wa Tanzania aone umuhimu wa kuanzisha Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ya Teknolojia, ili kuiandaa mahakama ambayo itahusika na mambo yaliyojitokeza kwenye teknolojia ikiwamo Akili Mnemba.

Mgombea Wakili Ibrahim Bendera alisema amedhamiria kuwaunganisha mawakili vijana na wale wa muda mrefu ili kuwasaidia kusimamia kuwajenga kitaaluma na kupata wateja.

“Kuna matatizo kwenye chama chetu mtu anakuuliza ni chama gani cha siasa, hakuna mwanasheria ambaye sio mwanasiasa tunachoangalia ni vigezo vya kitaaluma, mimi nikichaguliwa ndani ya chama sitaleta mambo ya huyu ni chama gani cha siasa tutafuata msingi wa Martin Luther,”alisema.

Mgombea mwingine ambaye ni Wakili Revocatus Kuuli, alisema akichaguliwa atazingatia masuala ya utawala wa sheria ikiwamo mgawanyo wa madaraka kwa dola, uhuru wa kutoa maoni ili kusaidia nchi bila vitisho na demokrasia kuwa na uchaguzi huru na haki.

Aliomba achaguliwe kwa kuwa amekomaa kuwa kiongozi mwenye msimamo na atakayesimamia uimara wa chama.

Mgombea Wakili Emmanuel Muga, anasema akichaguliwa atatengeneza mpango mkakati unaoendana na wakati wa sasa na atasimamia mafunzo na maadili ya Mawakili.

Alisema ataimarisha utawala kwa kutengeneza kamati zenye uwezo wa kufanya kazi na kuifanya TLS kufuata taratibu za kisheria na sio kuendesha mambo yake kiholela.

Mgombea Wakili Boniface Mwabukusi alisema “Mimi ni simba nitakayeongoza kundi la simba na watanzania wataanza kuona uwepo wa chama hiki kwa kuwa TLS ina wajibu kwa wananchi, serikali, wanachama na utawala wa sheria na mgawanyo wa madaraka katika mhimili ya dola.”

“Nataka kuleta umoja kwenye uwakili kwasasa umegawanyika, tunapokuwa na TLS yenye kuwajibika nchi zinavamiwa kiuchumi ni wajibu wa TLS kuongoza watanzania kujua ukweli wa kisheria wa mikataba ya kimataifa na sera tunazoingia,”alisema.

Previous articleRAIS SAMIA KUONGOZA MKUTANO WA 15 WA BARAZA LA TAIFA LA BIASHARA
Next articleNI KISHINDO CHA BALOZI NCHIMBI ZIARANI MTWARA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here