DAR ES SALAAM
Wabunifu bidhaa na vifaa mbalimbali nchini wametakiwa kulinda bunifu zao na kuzisajili kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili zisipotee au kutumiwa na watu wengine bila wao wenyewe kunufaika.
Wito huo umetolewa na Afisa Usajili kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Stansalaus Kigosi wakati akitoa mafunzo kwa walimu na wanafunzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam, Sabasaba.
Bw. Kigosi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kuwajengea uelewa wabunifu na wavumbuzi kutoka VETA kuhusu umuhimu wa kulinda kazi za ubunifu wanazozifanya katika kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii husika.
“Tunatambua kuwabkatika utatuzi wa changamoto mbalimbali kwenye jamii mmekuja na njia mbalimbali za kutatua changamoto, msiache bunifu zenu zikapotea bila kuzilinda” – alisema Bw. Kigosi.
“Michoro mnayoitengeneza inatakiwa kulindwa kabla ya kupeleka mitandaoni unajikuta unapeleka ubunifu wako bila wewe kunufaika.” aliongeza Bw. Kigosi
Naye Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA), Bw. Abdallah Ngodu amesema mafunzo hayo yatasaidia wabunifu wengi ambao wako katika taasisi yake kuweza kusajili kulinda bunifu zao kwani asilimia kubwa ya wabunifu hawajazilinda Miliki Ubunifu zao.
“Tunasisitiza sana ubunifu na lakini bado kumekuwa na changamoto kubwa kwenye kulinda bunifu zetu, wengi walikuwa hawafahamu hilo na mafunzo hayo yatawasaidia pia katika kufanya biashara na kupata manufaa zaidi.” alisema Bwa. Ngogu
BRELA inaelekea kutoa huduma za papo kwa papo katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam, Sabasaba kwenye banda lililopo karibu na Wizara ya Fedha na lililopo ndani ya Wizara ya Viwanda na Biashara.