Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga ACP Bernard Zacharia akizungumza na madereva bodaboda jijini Tanga baada ya kuhitimu mafunzo ya usalama barabarani
Na Mwandishi Wetu,Tanga
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga wamelipongeza Shirika la Amend na Ubalozi wa Uswiss nchini kwa kufanikisha mafunzo ya usalama kwa madereva bodaboda kwa Mkoa huo kwani yatawezesha madereva hao kufahamu sheria na kuzitii,hivyo kumpunguza ajali.
Akizungumza wakati akihitimisha mafunzo ya usalama barabarani, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga ACP Bernard Zacharia amesema wanatambua umuhimu wa mafunzo hayo kwa vijana wa bodaboda,hivyo wanatoa shukrani kwa Shirika la Amend na Ubalozi wa Uswiss nchini Tanzania kufanikisha mafunzo hayo kwa kushirikiana na na Jeshi la Polisi.
Amesema katika Wilaya ya Tanga madereva 204 wamepata mafunzo hayo na kusisitiza ni vema waliopata mafunzo wakawa mfano mzuri wa kuigwa sambamba na mabalozi kwa wenzao ili kwa pamoja wawe sehemu ya kukomesha ajali za barabarani.
Kamanda Zacharia amesisitiza Jeshi la Polisi linawahimiza watii sheria bila shuruti huku akiwashukuru Ubalozi wa Uswiss na Amend kwa ushirikiano wao na Jeshi la polisi kwa kuwaangalia vijana kwa ukaribu na kuwapatia mafunzo hayo.
Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani wanafahamu kuwa bodaboda wamekua wakisafirisha abiria na mali zao,hivyo mafunzo waliyoyapata madereva bodaboda hao wa Wilaya ya Tanga na maeneo mengine ya mkoa huo yatawasaidia wao na abiria wao kuwa salama.
“Tunatarajia bodaboda Mkoa wa Tanga mtakua mfano wa kuigwa na mtakuwa mabalozi wazuri.Jeshi la Polisi linawahimiza kutii sheria bila shuruti na tunawashukuru Ubalozi wa Uswiss na Amend kwa ushirikiano huu na Jeshi la polisi kwa kuwaangalia vijana kwa ukaribu huu.”
Awali Mratibu wa Shirika la Amend Ramadhan Nyanza amesema katika kipindi cha mwaka mmoja kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswiss nchini Tanzania ,- Shirika la Amend kwa kushirikiana na wadau mbalimbali limefanikiwa kutoa mafunzo kwa vijana zaidi ya 900 kwa mkoa wa Dodoma na Tanga.
Pia amesema wanaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na mashirika yasio ya kiserikali kuzifikia jamii. “Mafunzo ya usalama barabarani tunayatoa bure kwa vijana hivyo tunaomba waendelee kujitokeza wanaposikia fursa hizi kwani zinasaidia kuengeza pato lao binafsi na pato la taifa kwa ujumla kama maafisa usafirishaji.”
Mwisho