DODOMA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Madini iendelee kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kutafuta teknolojia mbalimbali za uongezaji thamani madini.
Amesema kuwa kufanya hivyo kutawezesha madini yanayopatikana nchini kutumika katika kuzalisha bidhaa ambazo zinahitajika duniani kote kutokana na kuongezeka kwa mahitaji na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watu duniani.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Juni 27, 2024) wakati alipofunga wiki ya madini iliyoambatana na Kongamano la Wachimbaji Madini, Mkutano Mkuu wa FEMATA pamoja na Maonesho ya Madini na Vifaa vya Uchimbaji iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa rai kwa Wafanyabiashara, Taasisi za Elimu, Taasisi za Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Madini kuendelea kuweka mikakati ya kuwezesha uwekezaji wa ndani wa teknolojia mbalimbali nchini zitakazowezesha upatikanaji wa malighafi zinazohitajika na migodi na shughuli nyingine za madini.
“Kwa kuwa teknolojia duniani inazidi kukua kwa kasi wadau wa madini waongeze na kuimarisha mtandao na wachimbaji wa kikanda na kimataifa. “Kwakujifungia ndani peke yetu hatutapata suluhisho lachangamoto tulizonazo bali tutachelewesha maendeleo yetu”
Amesema kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto, kero na adha zinazowakabili wawekezaji na wachimbaji wa madini pamoja na kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika ya kuuza madini pamoja na kuendelea kuwawezesha wawekezaji wadogo katika Sekta ya Madini kwa kuwaunganisha na Taasisi za Fedha nchini ili waweze kupewa mikopo.
“Katika hili nitoe wito kwa taasisi za Fedha nchini kukaa na FEMATA, wapeni miongozo na elimu ya mitaji ili waweze kuitumia katika kuzipa thamani kazi zao ili ziwe na tija”