Home LOCAL WANABUKOMBE WASISITIZWA KUWA NA SUBIRA KUHUSU PORI LA KIGOSI

WANABUKOMBE WASISITIZWA KUWA NA SUBIRA KUHUSU PORI LA KIGOSI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ardhi kueleza utaratibu kwa wananchi

Wananchi wasisitizwa kufuata utaratibu

 Wafuga nyuki kupewa vibali

 Dkt. Biteko asema yuko imara kuhakikisha anawaletea maendeleo Wanabukombe

BUKOMBE 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe lililopo mkoani Geita, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa wananchi wa Jimbo hilo kuwa na subira kuhusu kutumia Pori la Kigosi kufanya shughuli mbalimbali wakati ambao Serikali inaendelea kuandaa utaratibu maalum.

Ameyasema hayo Juni 6, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa soko la zamani uliopo Kata ya Igulwa Jimbo la Bukombe.

“Watu wema wa Bukombe naomba niwakumbushe historia ya Pori hili la Kigosi lenye ukubwa wa mita za mraba 13,000 ambalo lilikuwa Hifadhi ya Wanyamapori. Wakati nachaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo hili halikuwa na mahusiano mazuri kati yake na wananchi na wanaofuga nyuki walizuiwa kuingia katika pori hili na wakahoji kwanini nimewaletea kiwanda cha kutengeneza asali”,amesema Dkt. Biteko.

Amebainisha kuwa alimweleza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu changamoto hiyo ambapo alifanyia kazi kwa kuitisha vikao na hatimaye pori hilo lilishushwa hadhi na kuwa Hifadhi za Misitu za Taifa.

“ Hapa nataka tuelezane ukweli na hapa tupo na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Hifadhi za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amekuja lakini nyinyi mna haraka sana mambo haya yana utaratibu wake. Nimewaekeleza Waziri wa Maliasili na Utalii na Waziri wa Ardhi waje hapa kuwaeleza utaratibu ni upi”,amesema Dkt. Biteko.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Bukombe“ Nilimwambia Kamishna wa Uhifadhi awaambie askari wake kuwa uhai wa Watanzania una thamani kubwa hivyo wananchi wanaoingia huko bila kufuata utaratibu wafikishe kwenye vyombo vya sheria na washitakiwe. Hivyo, tusichokozane wanaoenda porini kwa michongo yaani bila utaratibu tusubiri kuelezwa na kufuata utaratibu”.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewataka wananchi wa Bukombe kulinda misitu huku akisisitiza kuimarisha uhusiano mwema kati ya wananchi na hifadhi, sambamba na kuwaeleza wafugaji wa nyuki kuendelea kufanya shughuli zao kwa kuwa na kibali maalum. Aidha, amesema kuwa ataendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha wananchi hao wanapata maendeleo.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Bw. Nicholaus Kasendamila akizungumzia suala la Pori la Kigosi amesema “ Serikali inaendelea na mchakato ili jambo hili lifike mwisho wananchi waweze kunufaika kutokana na shughuli za uchimbaji wa dhahabu hata hivyo nawashukuru TFS kuendelea kusaidia kutatua changamoto ya migogoro iliyokuwa inajitokeza”.

Ameendelea “Niwasihi pamoja na majibu ya Serikali tuwe na subira, tuheshimu sheria wakati tukisubiri Serikali itueleze kuhusu utaratibu ulioandaliwa.”

Pamoja na hayo, Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rose Busiga amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ambayo imetekelezwa ikiwemo ya hospitali, barabara na maji.

“ Pia, nimpongeze sana Mhe. Dkt. Biteko mbunge wetu kwa jitihada zake za kuhakikisha Bukombe inapata maendeleo kwa kutuletea miradi mbalimbali.” Amesema Mhe. Busiga.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here