Home LOCAL UMMY MWALIMU ANAVYOWAWEKEA WANAWAKE WA TANGA MAZINGIRA WEZESHI KIUCHUMI

UMMY MWALIMU ANAVYOWAWEKEA WANAWAKE WA TANGA MAZINGIRA WEZESHI KIUCHUMI

Na: Dk. Reubeni Lumbagala.

Uwezeshaji wanawake kiuchumi ni moja ya mikakati ya serikali yetu. Ni mkakati unaolenga kuwapa fursa za kumiliki mali na kuchangia maendeleo ya familia, jamii na taifa kwa ujumla. Kutokana na umuhimu wa wanawake katika jamii, hakuna namna ambayo familia, jamii na taifa linaweza kusonga mbele kimaendeleo kama kundi hili muhimu la wanawake litabaki nyuma bila kuweka mikakati thabiti ya kuwawezesha hasa katika nyanja ya kiuchumi ambayo kwa miaka mingi wanawake wamekuwa nyuma.

Tukumbuke usemi kwamba ukimwelimisha mwanaume, umeelimisha mtu mmoja lakini ukielimisha mwanamke umeelimisha jamii. Vivyo hivyo naamini ukimwezesha kiuchumi mwanamke, umewezesha jamii kubwa wakati kwa mwanaume unawezesha mtu mmoja.

Mtazamo wa kumwona mwanamke kama mtu wa kubaki nyumbani kulea familia tu bila kujishughulisha katika shughuli za uzalishaji mali unapaswa kubadilika kwani dunia imebadilika sana. Wanawake wamedhihiridha wana uwezo mkubwa wa kumudu majukumu ya uzalishaji mali na hatimaye kuchangia katika maendeleo ya familia na taifa.

Kwa kutambua umuhimu wa wanawake katika ujenzi wa taifa, Mbunge wa Tanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ambaye pia ni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati wa kujinadi kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, aliahidi kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuwainua wanawake kiuchumi na hatimaye kuharakisha gurudumu la maendeleo.

Ummy Mwalimu ameonesha na anaendelea kuonesha kwamba anatambua uwezeshaji wanawake kiuchumi una mchango mkubwa katika kupunguza umaskini na kuharakisha maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Moja ya mkakati ambao Mbunge huyu wa Tanga Mjini ameusimamia kikamilifu katika kuwainua wanawake ni uundwaji wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi wilaya ya Tanga. Uundaji wa jukwaa hili umekuwa na mafanikio makubwa kwani katika kata zote 27 za Jiji la Tanga, kumeundwa majukwaa haya, hii ina maana kuwa kila kata ina jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi.

Uwepo wa majukwaa haya kwenye kila kata unarahisisha ufikiwaji wa wanawake kule walipo na hivyo kuwawezesha kwa kuwapa semina na mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kushiriki shughuli za kiuchumi wakiwa katika vikundi vyao na pia kutoa mikopo itakayowasaidia kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Kuwatambua wanawake kule walipo na kupata taarifa zao ni muhimu katika kuhakikisha kuwa mikopo na mafunzo yanayotolewa yanawafikia walengwa husika na hivyo kuepuka uwepo wa vikundi hewa ambavyo ni hatari katika juhudi za kuwainua wanawake kiuchumi.

Ummy Mwalimu amejipambanua kuwa mlezi wa jukwaa la uwezeshaji wanawake Jiji la Tanga. Katika mkutano huo, Ummy amewawahakikishia kushiriki kwenye vikao vyao vya mara kwa mara, kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi ili juhudi za kuwainua wanawake kiuchumi katika Jiji la Tanga ziweze kufanikiwa kikamilifu.

Mei 17, 2024, Ummy Mwalimu alizindua rasmi Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Jiji la Tanga, hafla iliyofanyika katika ofisi za Halmashauri ya jiji la hilo.

Katika uzinduzi huo, Ummy amelitaka jukwaa hilo kuwalea na kuwasimamia vizuri wanawake wote katika ngazi za mitaa, kata na tarafa ili kwa pamoja waweze kuinuka kiuchumi.

“Na kwa upande wa jukwaa, nadhani Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Dada Aziza na Katibu wanajua kwenye shughuli za jukwaa nimekuwa nikishiriki na kila mwaka Siku ya Wanawake Duniani nimekuwa nikishiri kwa kuwa nipo pamoja na jukwaa. Mwenyekiti na timu yako sitawaacha, nitaendelea kufanya kazi na nyie kwa karibu sana kuhakikisha tunajiinua kiuchumi,” anasema Ummy Mwalimu.

Uwepo wa jukwaa hili ni muhimu katika kuwaunganisha wanawake pamoja kwa kuwapa mafunzo na mitaji ya kuwawezesha kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazowasaidia kukuza uchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Ummy anaona umuhimu wa kuwawezesha wanawake kiuchumi na ndiyo maana amemfananisha mwanamke na shingo katika mwili wa binadamu. “Kwa kweli tunasema baba ndiyo kichwa cha familia basi mwanamke ndiyo shingo, bila shingo kichwa hakiwezi kuwepo.”

Hii ina maana kuwa juhudi za baba peke yake katika kuinua uchumi wa familia haziwezi kuzaa matunda makubwa kama mama hatajishughulisha, lakini kwa pamoja (baba na mama) wakiunganisha nguvu, familia itasonga mbele kiuchumi kwa kasi kubwa. Na ikumbiukwe kwamba katika zama tulizo nazo tuna akina baba wanaotelekeza familia, wababa walevi na wasiojali mustakabali wa watoto wao na mfano wa hao.

Hali kadhalika kuna akina mama wajane na waliozalishwa kisha wahusika (wanaume) wakakana mimba au kukimbia majukumu. Wanawake hawa wote wanaotakiwa kuwezeshwa, si katika suala la mitaji pekee bali pia elimu ya uzalishaji mali, elimu ya biashara za kisasa ikiwemo matumizi ya intaneti na siku hizi akili mnemba, utendaji wa huduma za taasisi za fedha, utunzaji wa mahesabu hadi utafutaji wa masoko.

Ummy amewapongeza wanawake wa Tanga Mjini kwa jinsi wanavyojituma katika kujiongezea kipato ili kuboresha maisha yao na ya familia zao. Vilevile, amewasisitiza wanawake kutokata tamaa katika kujinyanyua kiuchumi na kujiunga kwenye vikundi rasmi vinavyotambulika ili kuweza kufikiwa kwa urahisi kupitia mikopo nafuu inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Mimi pia ninachukua fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa Ummy kwa kuwashika mkono wanawake hawa na kumhimiza asirudi nyuma katika kutoa mchango wake kuwanyanyua kiuchumi wanawake wa Tanga.

Katika uzinduzi huo, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahman Shiloow amesema serikali ina nia thabiti ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, kielimu na katika nyanja zote na ndiyo maana Jiji la Tanga lina majukwaa 27, ukiwa na maana kwamba kila kata ina jukwaa lake la kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Kwamba kila jukwaa katika kata linawajibika kupata elimu ya kutosha ili kuwajengea uwezo wanawake wa kata husika katika uchumi, elimu, afya na mazingira. Mstahiki Meya huyo wa Jiji la Tanga amesisitiza kuwa kipaumbele cha kwanza katika majukwaa hayo ni kujengewa uwezo wanawake kielimu na kujitambua, baadaye utoaji wa mikopo unafuata. Hii imekaa vizuri sana.

Aidha, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt. Frederick Sagamiko amemhakikishia Mbunge Ummy Mwalimu kuwa ushiriki wa wanawake wa Jiji la Tanga katika shughuli za kiuchumi ni mkubwa sana na wanapaswa kupongezwa. Mkurugenzi huyo amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameruhusu kuanzia Julai 1, 2024, mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri ianze kutolewa, na Jiji la Tanga limetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Ni wakati mwafaka kwa wanawake wa Jiji la Tanga kuyatumia vyema majukwaa hayo ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ili waweze kuinua vipato vyao kwa maendeleo. Ni vyema hatua kama ya Tanga ikasambaa nchi nzima. Kwamba mikoa mingine isione haya kwenda kujifunza Jiji la Tanga na kuanzisha majukwaa ya kuwawezesha wanawake katika kila kata kwenye maeneo yao.

Mara zote wanawake wakumbuke kuwa wao ndiyo shingo katika mwili wa uchumi, wakibaki nyuma, kichwa peke yake yaani baba atashindwa kufikia maendeleo ya kweli ya familia, hivyo basi, ni muhimu sana wanawake kusimama katika nafasi zao kwa kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa maendeleo endelevu ya familia, jamii na taifa. Mwanamke tafakari, chukua hatua leo.

Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462

Previous articleVIONGOZI WA BODI ZA VYAMA WATAKIWA KUTAMBUA WAJIBU WAO KATIKA VYAMA
Next articleMIAKA 60 YA MAPINDUZI NA MUUNGANO WA TANZANIA MAENDELEO NI MENGI-DK.MWINYI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here