Home LOCAL TAMKO KUHUSU HALI YA UCHUMI NA BAJETI KUU YA SERIKALI ILIYOWASILISHWA KWA MWAKA WA...

TAMKO KUHUSU HALI YA UCHUMI NA BAJETI KUU YA SERIKALI ILIYOWASILISHWA KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25

UTANGULIZI

Tamko hili ni jumla ya maoni ya Wanaharakati watetezi wa Bajeti Yenye Mrengo wa Kijinsia na Wadau wa Kongamano la Bajeti lililofanyika tarehe 13 na 14 Juni 2024, kuhusu  Hotuba ya Hali ya Uchumi na Bajeti ya Taifa zilizosomwa Alhamisi tarehe 13 Juni 2024, na Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Kitila Mkumbo pamoja na Waziri wa Fedha Mh. Mwigulu Nchemba.

Bajeti ya mwaka huu 2024/25 ni bajeti inayojengea kwenye mpango wa tatu wa maendeleo, ulioazimia kujenga uchumi shindani na shirikishi kwa maendeleo ya watu. Bajeti hii pia ndiyo inaenda kukamilisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya maendeleo 2025 na kutengeneza Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa 2050. 

Lengo la tamko hili ni kuwasilisha muhtasari wa uchambuzi uliofanywa na wanamtandao kuhusu mwenendo wa uchumi wa nchi na bajeti ya Taifa iliyowasilishwa (2024/25) kwa kuzingatia mahitaji na vipaumbele vya kijinsia. Dhamira yetu ni kutoa mapendekezo yanayojielekeza kuhakikisha nchi yetu inatumia vizuri rasilimali zilizopo kufikia usawa wa jinsia kwa kutumia nyenzo ya sera za bajeti na kodi ili kuziba mapengo ya kijinsia katika sekta mbalimbali za kijamii na uchumi kwa lengo la kuliletea taifa maendeleo endelevu, huku tukijenga uchumi shirikishi.

Tamko hili ni matokeo ya uchambuzi uliojikita katika kutathmini mambo matatu ambayo ni:

(i) Hatua zilizofikiwa kwenye utekelezaji wa bajeti 2023/24 katika kuleta usawa wa kijinsia na zilizoko katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025

(ii) Masuala ya Kijinsia yaayohitaji kuboreshwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025

(iii) Mapendekezo ya uboreshaji

Hatua zilizofikiwa kwenye utekelezaji wa bajeti 2023/24 katika kuleta usawa wa kijinsia na zilizoko katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025

Tunaona kuna baadhi ya hatua chanya ambazo nchi yetu inaendelea kupiga katika kuondoa tofauti na kuziba mapengo ya kijinsia katika sekta na huduma mbalimbali. Mfano: –

1.     Tunatambua na kuipongeza serikali kuu kwa kuingiza elekezo la kusistiza utengenezaji wa bajeti yenye mrengo wa jinsia katika muongozo wa bajeti ya mwaka 2024/25 katika kifungu na 4.5.6 (ukurasa wa 15), ambapo ilielekeza Wizara na Taasisi kuhakikisha inazingatia mambo 5 ili bajeti ziweze kuingiza na kuakisi masuala ya kijinsia. Baadhi ya mambo hayo ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha wizara na taasisi zinaainisha changamoto/masuala ya kijinsia kwa kufanya uchambuzi wa takwimu zilizonyambuliwa kijinsia na pili kuchukua hatua katika kuziba mapengo ya kijinsia yaliyobainishwa kupitia mipango na bajeti za taasisi husika. Hii ni hatua muhimu sana kwasababu imetoa agizo rasmi kwa watendaji kuhakikisha mipango na bajeti zao zinazingatia jinsia

 

 

2.     Sambamba na hii, tunapongeza jitihada na nia ya serikali za kutaka kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na uwekezaji unaoendelea wa kuhakikisha fedha zinazotumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo zinakuwa na tija katika kutatua changamoto za jamii na kuwafikia wafaidika waliokusudiwa. Hii tumeiona kwa serikali kuanzisha utaratibu mpya wa ufuatiliaji na kutathmini hatua za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuwa na taarifa za kila mwezi za matokeo yaliyopatikana kutokana na utekelezaji kupitia vitengo vya ufuatiliaji na tathmini vilivyoanzishwa ndani ya kila wizara na taasisi. Tunaamini utaratibu huu utasaidia katika kufanya tathmini ya mara kwa mara ya hatua zinazopigwa katika kuziba mapengo ya kijinsia kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutelezwa na serikali

 

3.     Kadhalika tunaipongeza serikali kwa kutoa tamko la kutaka maafisa masuhuli wa taasisi za serikali ambao hawatatoa asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalumu wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wawajibishwe na mamlaka husika. Hii itasaidia katika kuhakikisha kuwa taasisi zinazingatia agizo hili kwani utafiti uliofanyika na Tanzania Women Chamber of Commerce na TradeMark East Africa (2022) ulionesha kuwa asilimia 4 tu ya taasisi ndio zinatenga zabuni kwa utaratibu huu. Hatua hii ili kufikiwa ni muhimu kuwa na jitihada mahususi za kuhakikisha kuwa walengwa wa kupata zabuni hizo wanatambulika katika jamii na kuwezeshwa kiuchumi ili kukidhi vigezo za kupokea zabuni hizo.

 

4.     Uanzishwaji wa mfuko wa dharura wa kutengeneza miundombinu ya barabara zilizo haribika, kwani uharibifu wa barabara umekuwa ukisababisha ufikiwaji wa huduma za afya kwa mama wajawazito, wagonjwa mahututi kuwa ngumu pia zimekuwa zikihatarisha usalama wa watoto na wanafunzi wanaoishi vijijini wasiweze kufika au kwenda shule wakati wa mvua nyingi. Barabara zilizoharibika zimekuwa pia zikichangia wakulima hasa wanawake kushindwa kufikisha bidhaa zao masokoni kwa wakati na wakati mwingine kushindwa kabisa kwa sababu ya gharama za usafiri kuwa juu wakati wa mvua hivyo kulazimika kuuza mashambani kwa bei ndogo.

 

5.     Kuendelea kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwa kutoza kiwango cha asilimia 0 kwenye malighafi za kutengenezea taulo za kike pamoja na nepi za watoto kama sehemu ya makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki). Hii inaonesha nia ya kuendelea kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa taulo za kike hususani kwa ajili ya wasichana wanaotoka katika kaya maskini lakini pia katika kuhakikisha wanawake na wasichana hawaadhibiwa kwa kulipa kodi ya ziada sababu ya hitaji hili linalotokana na maumbile ya kibaolojia. Ili kupunguza mzigo mkubwa kwa wanawake na wasichana Serikali kuweka mfumo wa kufuatilia na kuhakikisha kuwa taulo za kike na za watoto zinashuka bei ili kiwango cha asilia 0 kinachotozwa kwenye ushuru wa forodha katika malighafi zinazozalisha taulo hizi kiwe na maana kwa mtumiaji wa mwisho.

 

6.     Kuendelea na jitihada za kutafuta pesa ya kugharamia bima ya afya kwa ajili ya watu wasio na uwezo na makundi maalum hususani wanawake wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Hii tumeiona kwa serikali kurekebisha Sheria ya ushuru wa bidhaa sura 147, ili kuelekeza asilimia 2 ya mapato ya bidhaa za urembo, vinywaji laini na vileo kwenye bima ya afya kwa wote hatua ambayo itaongeza kiasi kidogo cha shilingi milioni 18 na laki nane tu, katika mfuko huo (ukurasa wa 98, Hotuba ya Bajeti ya Taifa). Hata hivyo licha ya kwamba tunaitambua hii ni hatua, tunaona bado kiasi kinachotokana na vyanzo tajwa ni kidogo kwa hiyo serikali ingeweza kufikiria maeneo mengine zaidi kama vile kwenye sigara, michezo ya kamari na bahati nasibu pamoja na mpira wa miguu.

 

MASUALA MUHIMU YA KIJINSIA YANAYOHITAJI KUBORESHWA

Pamoja na masuala mazuri yaliyopo kwenye bajeti hii, ni dhahiri kuwa bado kuna maeneo ambayo ziko changamoto na mapungufu yanayohitaji kutazamwa kabla ya Bajeti hii kupitishwa kama ifuatavyo:

  1. Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa fedha, uwiano wa mapato ya kodi kwa Pato la Taifa umeongezeka kutoka 12.5% ​​ya 2023/24 hadi 12.8% mwaka 2024/25. Hii inamaana kuwa mchango wa mapato ya kodi katika Pato la Taifa umeongezeka kwa asilimia 0.3 tu. Kuwekeza katika kufikia usawa wa jinsia ni ndoto endapo wigo wa mapato hasa ya kodi hautakuwa unaongezeka. Mfano, Tangu 2015/16 hadi 2023/24, uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa umebakia kuwa wa wastani wa asilimia kumi na mbili (12%). Lakini kwa kweli utoaji wa huduma za kijamii na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi utakuwa na ufanisi ikiwa mapato ya kodi yatachangia angalau 35% kwenye Pato la Taifa (GDP) kulingana na vigezo vya OECD.

 

  1. Kupungua kwa kiwango cha bajeti ya taifa ambayo imeelekezwa katika sekta za huduma za kijamii, kama vile elimu, afya na maji. Tumeona kuwa fungu la sekta ya elimu kwa bajeti ya taifa imeendelea kupungua kutoka 13.7% (2022/23), 13.4% (2023/24) hadi kufikia 12.5% (2024/25). Kadhalika fungu la bajeti ya sekta ya afya imeendelea kutotabirika kutoka 5.2% (2022/23), 5.5% (2023/24) hadi 5.1 (2024/25), kadhalika kwenye sekta ya maji imepungua kutoka 1.72% (2023/24 hadi 1.3% (2024/25).

 

Mwenendo huu hauakisi mabadiliko, vipaumbele, wala mahitaji halisi ya sekta hizi za kijamii ambazo ndio msingi wa mapinduzi ya kiuchumi. Mfano bajeti ya sekta ya elimu ni shilingi trilioni 6.166. Kiwango hiki cha bajeti ni kidogo kuliko kiwango cha juu ambacho kilikadiriwa cha trilioni 6.3 kwa mwaka 2020/21 kutekeleza mpango wa maendeleo ya elimu (ESDP 2017/18-2020/21) licha ya kwamba sekta ya elimu imeanza kutekeleza mtaala mpya wenye kuhitaji uwekezaji mkubwa. Hali hii inatia shaka endapo baadhi ya programu za elimu kama vile ya kurudisha shule wanafunzi waliotoka kwenye mfumo rasmi wa elimu kwa changamoto mbalimbali, pamoja na uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia ya wanafunzi wenye ulemavu zinaweza kutekelezwa kiufanisi.

 

  1. Matumizi ya serikali katika sekta mbalimbali za uchumi hayajawa na athari chanya katika kuondoa kundi kubwa la watanzania wa kipato cha chini kwenye lindi la umaskini. Kulingana na hotuba ya waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ukurasa wa 18, “ukuaji wa uchumi umekuwa ukihusisha sekta chache na ambazo haziajiri watu wengi kutoka kaya maskini. Sekta zilizoongoza kwa ukuaji kwa mwaka 2023 ni pamoja na Sanaa (17.7%), fedha na bima (12.2%), madini (11.3%) na malazi na chakula (8.3%).  Sekta ambazo zilitarajiwa kuajiri watu wengi zilikua kwa kasi ndogo. Sekta hizi ni pamoja na kilimo (4.2%), viwanda (4.3%) na biashara (4.2%). Matokeo ya hali hii ni kwamba ukuaji wa uchumi umekuwa hauendani na kasi ya kupunguza umaskini kwa kiwango cha kuridhisha.”

 

Hii inamaanisha kuwa, kwa mfano licha ya kwamba serikali inatumia fedha nyingi katika sekta ya kilimo, ambayo ni takriban  asilimia tatu ya bajeti ya taifa, Trilioni 1.2 (2022/23), Trilioni 1.46 (2023/24) na trillion 1.94 (2024/25), bado utekelezaji wa programu za kilimo ama hauwafikii walengwa kwa kiasi inachopaswa au afua zinazotekelezwa sio sahihi hivyo kufanya hali ya uchumi ya wananchi walio wengi walioajiriwa na sekta hii kutokwamuka kiuchumi, na hapa tunazungumzia kundi kubwa la wanawake na vijana na wanaume walioko pembezoni kutoka kwenye kaya maskini kwa kuwa kulingana na waziri “Uchumi unakuwa kwa kasi zaidi mijini kuliko vijijini” ukurasa 19. Hii inatuambia kuwa ijapokuwa uchumi unasemekana kuendelea kukua kwa kasi nzuri (5.1%), ukuaji huu sio shirikishi kama ambavyo Mpango wa III wa maendeleo unavyotaka, “kuchochea uchumi shindani na shirikishi”, kwa hiyo badala ya kuchangia katika kuziba pengo la jinsia katika kipato aina hii ya matumizi inaweza kuendeleza hilo pengo la jinsia kwa muda mrefu, kadhalika kukwamisha ukuaji wa sekta hii kufikia 10% kwa mwaka ifikapo 2030.

  1. Idadi ya vijana wanaofaidika na mikopo ya kilimo kupitia programu ya BBT ni kidogo ukilinganisha na uhitaji uliopo licha ya kwamba kulingana na hotuba ya hali ya uchumi mikopo katika sekta ya kilimo iliongezeka kwa kasi kubwa katika mwaka 2023/24. Mfano taarifa zinaonesha kuwa kumekuwa na ukuaji wa kasi wa mikopo katika sekta ya kilimo kutoka 44% (2022/23) hadi 60.6% (2023/24). Hata hivyo katika hotuba ya waziri wa kilimo inaonesha kuwa vijana waliopata mikopo ya BBT yenye riba chini ya 4.5% katika mwaka wa fedha 2023/24 walikuwa ni 118 tu, ambapo mikopo hiyo ilikuwa na thamani ya shilingi milioni 950.09. Pamoja na kuwa idadi ni ndogo, takwimu hizi hazijanyambuliwa vya kutosha kutoa fursa ya umma kujua katika hawa walionufaika wangapi walikuwa wasichana na wangapi wavulana, hivyo kufanya iwe vigumu kujua kama programu ya BBT inazingatia pengo lililopo la jinsia katika utekelezaji wake.
  2. Mkakati wa serikali wa kutegemea wahisani au wadau wa maendeleo kwa ajili ya kupata fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi sio endelevu kwani masuala ya mabadiliko ya tabia nchi yanahitaji utatuzi wa papo kwa hapo kwasababu ya athari zake kwa wananchi husasani suala la usalama wa chakula. Kulingana na hotuba ya waziri wa fedha (ukurasa wa 57), “Kwasasa serikali iko katika majadiliano na shirika la fedha la kimataifa (IMF), ili kunufukaika na mkopo nafuu kupitia dirisha la Resilience and Sustainability Facility, kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi”. Utegemezi huu wa fedha za nje ambazo hazitabiriki ili kukabiliana na changamoto kama hii sio mbadala sahihi.
  3. Kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye malighafi za kuzalisha taulo za kike na nepi za watoto haitoshi kuhakikisha kuwa gharama za taulo hizi anazolipa mtumiaji wa mwisho zinapungua. Hii inatokana na kwamba pamoja na kwamba hatua hii imechukuliwa, serikali haijawa na mkakati wa kuhakikisha kuwa wasambazaji na wauzaji wa bidhaa hizi wanashusha bei kulingana au sawasawa na kupungua kwa gharama za uzalishaji ambazo zinakuwa zimejitokeza baada ya kupewa unafuu wa ushuru wa forodha. Mfano, Serikali ilitamka kuondoa VAT kwa taulo za kike lakini haikuwa na matokeo katika bei za mwisho, lakini hili lilitokana kutokuwepo utaratibu wa ufuatiliaji kuhakikisha bei zinashuka za hii bidhaa.

 

 

 

MAPENDEKEZO YA MABORESHO

Kulingana na changamoto tulizobainishwa hapo juu tunashauri yafuatayo: –

  1. Serikali kutoa elekezo kwa Wizara na Taasisi kutoa Gender Budget Statement (GBS), kama sehemu ya uwajibikaji katika utekelezaji wa masuala ya kijinsia katika afua na mradi mbalimbali ambayo itakuwa inawasilishwa kwa Wizara ya Fedha na Maendeleo ya Jamii, kila wakati wanapotoa taarifa za utekelezaji. Hii itasaidia kuona ikiwa agizo lililoko katika muongozo wa bajeti kuhusu kuandaa bajeti zenye mrengo wa kijinsia linazingatiwa katika utekelezaji

 

  1. Serikali iendelee kutafuta vyanzo vipya vya mapato ya kikodi ambazo sio kandamizi ili kukidhi mahitaji na huduma zitakazowafikia makundi yote kwa usawa. Bajeti ya 2024/2025 inaonesha kuwa kati ya fedha nyingi zitakazokusanywa zitatumika katika kulipa deni la serikali, kumalizia miradi mikubwa ya kimkakati na kuandaa mashindano ya “AFCON”. Kwa sasa njia kubwa za makusanyo zinategemea fedha zinazokusanywa kutoka mamlaka ya kukusanya kodi (TRA) na vyanzo hutoka Halashauri huku gharama za maisha zikiwa zikipanda na kuwepo kwa ongezeko kubwa la mfumuko wa bei. Kwa kuchukua mfano wa wafanyakazi walioajiriwa, mishahara haijaongezeka viwango kukidhi mahitaji kwa wale wanaokatwa “PAYE” hivyo hali hii inaweza kuleta ongezeko kubwa la Ukatili wa kijinsia linaloambatana na changamoto za afya ya akili wahanga wakubwa wakiwa ni wanawake, wasichana na Watoto.

 

  1. Ongezeko la bajeti za sekta za huduma za afya ziendane na ongezeko la idadi ya watu nchini kadhalika ziakisi mabadiliko ya kisekta yanayoendelea (sector reforms), ili kuhakikisha tunafikia malengo ya maendeleo kulingana na Dira ya taifa 2025 ya kuwa na “Maisha bora na mazuri kwa kila mtanzania, na kuwa na jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza”

 

  1. Kutoa motisha na hamasa za kikodi na mitaji, kufungua fursa na kulegeza masharti ya kuanzisha biashara katika sekta zinazoendelea kukua kwa kasi zaidi  ili kundi kubwa la nguvu kazi ya taifa (vijana na wanawake) waweze kujiajiri au kuajiriwa.

 

  1. Kuongeza jitihada za uwekezaji katika kusaidia wanawake,vijana na wakulima wadogo kushiriki katika kuongeza si tu uzalishaji lakini pia uongezaji wa thamani ya bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi

 

  1. Kutoa hamasa kwa wanawake wakulima washiriki katika uzalishaji wa mazao ya biashara yenye tija kipato kwa kutoa ruzuku maalumu za pembejeo, zana za kilimo, mitaji, elimu ya biashara na uhakika wa masoko kwa vikundi

 

  1. Taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinazotajwa kama mafanikio zinazoingizwa kwenye hotuba ziwe zinaonesha idadi ya wanufaika kwa jinsi, na matokeo ya viashiria vyenye mrengo wa kijinsia wa shughuli zinazoendelea au zilizotumika katika utekelezaji
  2. Tunahimiza wizara na taasisi zake kuhakikisha zinatumia takwimu mbalimbali zilizonyumbuliwa kijinsia pamoja na tafiti za masuala ya kijinsia wakati wa kutengeneza mipango yao ya mwaka, hii itahakikisha kuwa na afua za miradi ambazo zimejielekeza katika kufikia makundi yaliyoachwa nyuma zaidi mfano wanawake na watu wenye ulemavu.
  3. Tunatoa rai kwamba fedha zilizotengwa kwa ajili ya uchaguzi zitumike kutetea haki za raia wote, kwa kuzingatia hasa suala la ulinzi na uwezeshaji wa makundi yote ambayo yamekuwa yakiathirika na mazingira ya uchaguzi yasiyo mazuri. Hii itasaidia kuhakikisha kuwa wanawake, wasichana, watoto, wazee, watu wenye ulemavu na makundi mengine ya kijinsia wanaweza kushiriki katika mchakato wa uchaguzi, kama wapiga kura na wagombea.
  4. Mwisho tunasistiza kuwa rasilimali zilizotengwa za kuwezesha mchakato wa kupokea maoni ya wananchi kuhusu dira ya Taifa 2050, zitumike kuwafikia zaidi wananchi walioko katika maeneo yote hasa yaliyopembezoni na makundi maalumu hususan wanawake, watu wenye ulemavu, na vijana wa kike kwa wa kiume, na walioko katika sekta mbalimbali kwa misingi ya usawa.

 

 
Previous articleRAIS SAMIA AVITAKA VYOMBO VYA HABARI KUHAMASISHA UPOKEAJI WA UJUZI MPYA
Next articleBENKI YA TCB YATANGAZA FAIDA YA SH. BILIONI 19.27
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here