Home SPORTS MAJALIWA: SERIKALI ITAENDELEA KUIPA KIPAUMBELE SEKTA YA MICHEZO

MAJALIWA: SERIKALI ITAENDELEA KUIPA KIPAUMBELE SEKTA YA MICHEZO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa sekta ya michezo inaendelea kuwezeshwa na kupewa kipaumbele kwa kuwa ni sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Amesema kuwa sekta hiyo inachangia kutoa ajira kwa vijana, kuchangia pato la Taifa, inapunguza gharama za matibabu kwa maradhi yasiyoambukiza, inalitangaza Taifa Duniani, inaleta burudani na hamasa pamoja na kujenga umoja wa kitaifa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumapili, Juni 9, 2024) kwenye Hafla ya Tuzo za Michezo katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar Es Salaam, ambapo amesisitiza matumizi sahihi ya fedha zinazotengwa kwa shughuli za michezo.

“Fedha inayotengwa kwa ajili ya shughuli za michezo hususan asilimia tano ya Mfuko wa Maendeleo ya Michezo itumike kama ilivyokusudiwa ili kuendelea kuinua michezo nchini.“

Waziri Mkuu amesema katika kipindi hiki imeshuhudiwa ongezeko kubwa la bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambapo kwa mwaka ujao wa 2024/2025 kutakuwa na ongezeko la kutoka shilingi bilioni 35.4 mwaka 2023/2024 hadi kufikia bilioni 285.3 sawa na ongezeko la asilimia 805.

“Hili ni ongezeko kubwa zaidi kuwahi kutokea tangu kuanzishwa kwa Wizara hii. Tumpongeze na kumshukuru sana Mhesimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuthamini michezo na utamaduni.“

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iandae programu mbalimbali za michezo ambazo zitakuza vipaji kwa Watanzania kuanzia ngazi ya elimu ya awali.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara ihakikishe inashawishi uwekezaji katika viwanda vya vifaa vya michezo hapa nchini ili vifaa vya michezo vyenye ubora viweze kupatikana kwa wingi na kwa bei rafiki.

“Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zihakikishe michezo inachezwa kikamilifu katika ngazi zote za shule ikiwemo ya Awali, Msingi, Sekondari pamoja na Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati.”

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wadau wote wa michezo kama walivyoainishwa katika sera ya maendeleo ya michezo wahakikishe wanashiriki katika kuendeleza michezo ipasavyo.

Previous articleSOMA MAGAZETI YA LEO JUMATATU JUNI 10-2024
Next articleWANNE WAKAMATWA WAKITOROSHA MIFUGO 70 KWA NJIA ZA PANYA ROAD LONGIDO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here