Home BUSINESS BoT, TAMISEMI KUBORESHA MIKOPO HUDUMA NDOGO ZA FEDHA

BoT, TAMISEMI KUBORESHA MIKOPO HUDUMA NDOGO ZA FEDHA

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inashirikiana na TAMISEMI katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya huduma ndogo za fedha nchini, hususan huduma za mikopo, ili kuiwezesha sekta hiyo kuwa na manufaa kwa wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa semina kwa wabunge iliyofanyika katika ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa BoT imefanya juhudi kubwa kwa kushirikiana na TAMISEMI ambapo maafisa maendeleo ya jamii na maafisa biashara wanajengewa uwezo ili kuwatambua wale wanaokopeshana bila leseni na kuwachukulia hatua stahiki.

“Tumetengeneza mwongozo ambao tutatoa mwezi Julai mwaka huu, ukiainisha mambo ya kufanya na adhabu kwa wanaokiuka sheria. Katika kila ngazi ya kata na wilaya, wanaokopesha watakuwa na vikao vya kukutana na kupeana taarifa kuhusu wale wanaokiuka taratibu,” alisema Tutuba.

Gavana alieleza kuwa mikopo mingi inatozwa gharama kubwa zisizoeleweka kama vile ada ya fomu, ada ya kushughulikia mkopo, na ada ya mkopo. Alisema mwongozo mpya utakaotolewa utadhibiti gharama hizi zote ziwe sehemu ya ada ya mkopo pekee.

“Kuna baadhi ya wakopeshaji wanaweka riba na gharamq za bima zisizoeleweka, lakini miongozo itadhibiti gharama za ziada zisiwe sehemu ya mkopo. Pia, watatakiwa kuwasilisha viwango vyao vya riba BoT kwa ajili ya kuviidhinisha na vitatumika kwa mwaka mzima,” aliongeza.

Kwa upande wa wakopaji, Gavana amesema kuwa changamoto kuu ni kutokurejesha mikopo kwa wakati, huku wakopeshaji wakikosa uwazi wanapokosesha. “Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma, ikiwemo kuingiza mada za elimu ya fedha katika mitaala rasmi ili kuhakikisha watu wanapohitimu shule wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha” alisema.

Gavana Tutuba alisisitiza kuwa BoT inaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wanaokiuka sheria, ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya leseni na kuwapeleka mahakamani.

Akiwasilisha mada kuhusu mfumo wa Sera ya Fedha unaotumia riba, Meneja Msaidizi, Kurugenzi ya Utafiti na Sera za Uchumi BoT, Dkt. Lusajo Mwankemwa, amesema kuwa kuanzia Januari 2024, Benki Kuu imeanza kutoa mwelekeo wa riba itakayotumika katika soko la fedha baina ya mabenki, badala ya kutumia ujazi wa fedha.

“Mabadiliko katika riba hiyo yanaashiria mwelekeo wa Sera ya Fedha katika kuhakikisha kuwa ukwasi katika Uchumi unaendana na malengo ya kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa Uchumi,” alisema.

Dkt. Mwankemwa aliongeza kuwa Mfumo wa kutumia riba katika kutekeleza Sera ya Fedha ni miongoni mwa mifumo inayotumika kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa Uchumi. Ili mfumo huu uweze kuleta ufanisi katika kufikia malengo yaliyokusudiwa, ni muhimu kufanya kazi pamoja na sera nyingine za Uchumi.

Semina hiyo ilifanyika chini ya uenyekiti wa Mhe. Twaha Ally Mpembenwe (Mb) akiwepo pia Kamishna Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here