Home LOCAL WATUMISHI MBEYA WAPEWA MATUMAINI KUHUSU KIKOKOTOO

WATUMISHI MBEYA WAPEWA MATUMAINI KUHUSU KIKOKOTOO

Mkuu wa Wilaya aya Rungwe Mhe. Jaffar Haniu amesema kutokana na mchango mkubwa wanaoutoa wafanyakazi mkoa wa Mbeya na Taifa kwa ujumla, madai yao kwa Serikali kuangalia upya suala la kikokotoo litafikishwa mahali sahihi kwakuwa Serikali ya Awamu ya Sita ni sikivu na inawajali wafanyakazi.

Mhe. Haniu ameyasema hayo tarehe 1 Mei, 2024 akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, wakati wa Sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, yaliyofanyika kimkoa wilayani Rungwe.

” Tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani imekuwa ikiboresha mazingira ya kazi na kuwezesha wananchi wake kuingia kwenye mfumo rasmi wa ajira serikalini, katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, hii inadhihirisha wazi kuwa inawajali wananchi wake”, amefafanua Mhe. Haniu.

Ameeleza zaidi kuwa Serikali imeruhusu kuendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, mkoa wa Mbeya ukiwa umetengewa shilingi Bilioni 5.

Pamoja na hayo Mhe. Haniu amewataka wafanyakazi kupinga na kukemea vitendo vya rushwa katika maeneo ya kazi kwani palipo na rushwa haiwezi kupatikana huduma bora.

Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi, Mratibu wa Chama cha Wafanyakazi TUCTA, Bw. Riziki Mashaka alisema mtumishi hufanya kazi kwa muda mrefu bila ongezeko la mshahara wenye tija, kutokana na hali hiyo hustaafu akiwa na kiasi kidogo cha fedha na kusababisha ugumu wa maisha kwa mtaafu huyo.

Amesema pia kuwa kikokotoo kinamfanya mfanyakazi kupata fedha kidogo mara tu, anapostaafu kwa kupata asilimia 33 ya kile alichopaswa kukipata, hivyo ameiomba Serikali kuboresha utoaji huduma kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ili wanufaika wapate stahiki zenye tija zitatakazo wasaidia kwenye kustaafu kwao, huku akitolea mfano kwa Wabunge wanaolipwa stahiki zao mara tu, wanapomaliza muda wao wawapo bungeni zaidi ya shilingi milioni 270 ikiwa ni nje ya mshahara wa kila mwezi.

Bw. Mashaka amesema kuna haja ya Serikali kubadili kanuni ili kunufaisha wafanyakazi na kuendelea kuimarisha zaidi mifuko ya jamii .

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here