Home LOCAL WANANCHI WATAKIWA KURIPOTI MATUKIO YA UKATILI WA KIJINSIA

WANANCHI WATAKIWA KURIPOTI MATUKIO YA UKATILI WA KIJINSIA

Wananchi wa Wilaya ya Mbeya na mkoa kwa ujumla wametakiwa kuacha tabia ya kumaliza changamoto za masuala ya ukatili wa kijinsia kifamilia na badala yake kufikisha katika vyombo vya sheria, ili kukomesha matukio ya aina mbalimbali ya ukatili kwenye jamii.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya katika Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, yaliyofanyika kwenye Stand ya mabasi, Mamlaka ya Mji Mdogo Mbalizi, leo tarehe 15 Mei, 2024, amewataka wananchi kufikisha kwenye vyombo vya sheria ukatili wowote wa kijinsia ili kutokomeza tabia hiyo inayoweza kusababisha kuwa na kizazi katili endelevu.

Aidha Mhe. Malisa amewasihi wananchi kumaliza tofauti za kifamilia zilizopo kwa amani ili kuboresha ustawi wa watoto na familia.

“Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za masuala ya ukatili zinaonesha baadhi ya matukio yanasabishwa na visasi vinavyotokana na kushindwa kutatua changamoto zinazowakabili kati yao”, amefafanua Mhe. Malisa. 

Mhe. Malisa ameeleza kuwa hali ya ukatili hujitokeza panapokuwa na migogoro ya kifamilia kwa wazazi kushindwa kuelewana na kuzalisha watoto wa mitaani wanaoishi kwenye mazingira magumu na kupelekea kuzalisha makundi ya uhalifu katika jamii.

“Ninawaomba wananchi amani na upendo vitawale na muweze kumaliza tofauti zenu kifamilia bila migogoro na matatizo kwa watoto”, amesisitiza Mhe. Malisa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Wilaya ya Mbeya Bw.Joseph Lusoko amesema matukio ya ukatili kwa sasa yanatolewa taarifa tofauti na siku za nyuma jambo ambalo linaonesha kiwango cha elimu na uelewa juu ya mapambano dhidi ya ukatili kimeongezeka.

Maadhimisho ya Siku ya Familia hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 15 Mei ambapo mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Tujaribu kumaliza tofauti zetu ndani ya familia ili ustawi wa watoto na familia zetu uwe mkubwa”.

Previous articleWATUMISHI FCC WAJENGEWA UWEZO NA UELEWA MPANA KUHUSU UENDESHAJI BIASHARA NA UCHUMI KATIKA MTANDAO 
Next articleTANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA KIDIPLOMASIA WA UKAMILISHWAJI SHERIA YA KIMATAIFA YA MILIKI UBUNIFU
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here