Home LOCAL MBEYA YAJA NA MKAKATI WA CHAKULA NA LISHE BORA KWA WANAFUNZI

MBEYA YAJA NA MKAKATI WA CHAKULA NA LISHE BORA KWA WANAFUNZI

MBEYA

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa amewataka wadau na jamii Mkoani Mbeya kuhamasisha suala la uchangiaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni ili kukuza kiwango cha ufaulu Mkoani Mbeya.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tarehe 2 Mei, 2024 kwenye kongamano la lishe lililofanyika katika ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya, Mhe. Malisa amesema kila mmoja kwa nafasi yake ahimize kuhusu uchangiaji wa chakula shuleni na kama wilaya na wadau wakitimiza wajibu kwenye suala hili basi jamii itakuwa imenufaika kwa kiasi kikubwa.

Mhe. Dormohamed Issa Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya amesema Serikali kupitia Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia suluhu Hassan amelipa kipaumbele suala la lishe ili kujenga taifa lenye watu wenye afya bora na imara.

Aidha Afisa Lishe Jiji la Mbeya Bi. Itika Mlagalila amebainisha kuwa mototo asipopata huduma ya chakula awapo shuleni inasababisha kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango chake cha ufaulu na uelewa awapo darasani, hivyo wazazi wanapaswa kuchangia chakula kusaidia kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Bw. John Nchimbi amesema lishe ni jambo la msingi kwa afya na viongozi wamekuwa wakifanya jitihada kuhamasisha suala la lishe.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kagera iliyopo jijini Mbeya, Bi.Sarah Maganga amesema wao kama walimu wamekuwa wakifanya jitihada za kutosha kuhakikisha wazazi wanachangia chakula kwa kuwapa elimu na kongamano hilo litakwenda kuongeza chachu zaidi kwa jamii kuona umuhimu walishe shuleni.

Mwalimu Maganga anaendelea kusema kuwa japo jitihada kubwa inafanyika bado changamoto inayojitokeza ni wazazi kuhisi walimu wanajinufaisha kwa michango inayotolewa na wazazi, kitu ambacho kinaleta ugumu katika kufanikisha zoezi hilo.

Mwakilishi kutoka Shirika la Helvetas, linalosimamia maradi wa kuimarisha mifumo ya chakula ndani ya Jiji la Mbeya, Bi. Judith Sarapion amesema kuwa wao kama wadau wakuu wa uwezeshaji wa shughuli za lishe Jiji la Mbeya, watahakikisha wanafunzi wanapata chakula wawapo shuleni ili kuimarisha afya zao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here