Home BUSINESS BRELA KUADHIMISHA SIKU YA MILIKI UBUNIFU DUNIANI MEI 9, 2024 JIJINI DAR

BRELA KUADHIMISHA SIKU YA MILIKI UBUNIFU DUNIANI MEI 9, 2024 JIJINI DAR

Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Loy Mhando akizungumza katika Mkutano wa Waandishi wa habari, kuhusu maadhimisho ya siku ya Miliki Ubunifu Duniani yatakayofanyika Mei 9, 2024, Jijini Dar es Salaam. (Kulia), ni Neema Kitala, Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Hataza , kurugenzi ya Miliki Ubunifu – BRELA.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma  (BRELA),  Theresa Chilambo, akizungumza alipokuwa akitoa neno la ukaribisho kwa waandishi wa habari katika mkutano huo, uliofanyika leo Mei 9, 2024, kwenye Ofisi za Wakala huyo, Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Miliki Bunifu (BRELA), Loy Mhando, (katikati), akifafanua jambo alipokuwa akijibu maswali ya Waandishi wa habari katika mkutano huo. (kushoto), ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma (BRELA),  Theresa Chilambo, na (kulia), ni Neema Kitala, Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Hataza , kurugenzi ya Miliki Ubunifu – BRELA.

(PICHA NA: HUGHES DUGILO)

Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM 

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya siku ya Miliki Ubunifu Duniani, yatakayofanyika kesho Mei 09, 2024 Jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yatafanyika katika Hotel ya Johari rotana Jijini humo, ambapo yanatarajiwa kuudhuriwa na wadau mbalimbali pamoja na viongozi wengine akiwemo Naibu waziri wa utamaduni, sanaa na michezo, Hamis Mwinjuma.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Miliki Bunifu Loy Mhando, amesema maadhimisho hayo yalianzishwa na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO), ambapo huadhimishwa Aprili 26 kila mwaka Duniani kote, lakini kwa Tanzania huadhimishwa tarehe tofauti kutokana na tarehe husika kuwa na jambo muhimu la Kitaifa la kuazimisha muungano wa Tanzania Bara. 

Aidha katika maadhimisho hayo kutakuwa na matukio mbalimbali yatakayoambatana nayo ikiwemo mijadala kuhusu Miliki Ubunifu ambayo itahusu fursa, mafanikio na changamoto wanazokutana nazo kwenye eneo zima la Miliki Ubunifu.

Ameongeza kuwa katika maadhimisho hayo, hati za makubaliano ya ushirikiano katika eneo la Miliki Ubunifu baina ya BRELA, COSOTA na Taasisi nyingine zitasainiwa. “Makubaliano hayo ni njia ya kurasimisha ushirikiano uliopo baina ya Taasisi hizo, katika kuhakikisha Miliki Ubunifu inaleta manufaa katika maendeleo ya kiuchumi na teknolojia nchini” ameongeza Loy.

Aidha amesema Miliki Ubunifu inatija kubwa kwa wabunifu ambapo inawapa ulinzi wa kumiliki bunifu zao na kuwasaidia katika kupata haki zao endapo mtu yoyote ataingilia ama kutumia bunifu yake pasipo makubaliano na mmiliki.

BRELA inawaalika wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taasisi zinazosimamia masuala ya Miliki Ubunifu Tanzania Bara na Zanizabar, Taasisi za umma pamoja na sekta binafsi, ili kujadili kwa pamoja fursa, mafanikio, na changamoto zolizopo katika nyanja ya Miliki Ubunifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here