Katika utekelezaji wa Sera yake ya Uwekezaji kwenye Jamii, Benki ya CRDB imeendelea kusaidia jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya elimu nchini.
Jitihada hizo zimefanyika mkoani Manyara, katika Wilaya za Mbulu na Babati, siku chache kabla ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Benki ya CRDB uliofanyika jumamosi ya tarehe 18 Mei 2024
Baadhi ya shule zilizonufaika na uwezeshaji huo ni Shule za Msingi shikizi Muungano ya Babati Mjini iliyokabidhiwa madarasa Mawili na Ofisi ya Walimu na shule ya Endagikot iliyoko wilayani Mbulu iliyokabidhiwa Darasa na madawati kwaajili ya Watoto wenye uhitaji malumu.
Misaada ya madarasa kwa shuke za msingi shikizi Muungano yalikabidhiwa na Mkurugenzi wa Manunuzi Benki ya CRDB, Pendason Philemon tarehe 14 Mei 2024 na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga ambaye aliishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huo unaounga juhudi za serikali kuboresha sekta ya elimu nchini.
Aidha, tarehe 15 Mei 2024, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Frederick Nshekanabo alikabidhi darasa kwa ajili ya Watoto wenye mahitaji maalumu kwa Shule ya Msingi Endagikot iliyopo wilaya ya Mbulu na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya wa Manyara, Mhe. Lazaro Twange ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara ambaye aliishukuru Benki ya CRDB kwa mara nyingine kuchangia ukuaji elimu katika Mkoa wa Manyara.
Ujenzi wa madarasa hayo ni sehemu ya utekelezaji wa sera yetu ya uwekezaji kwa Jamii (Policy) inayotenga asilimia moja ya faida ya benki kila mwaka kuwezesha miradi ya maendeleo katika jamii.
Benki pia inatekeleza mradi wa Keti Jifunze unaolenga kutatua changamoto za elimu zinazojumuisha upungufu wa madarasa na ofisi za walimu, madawati, vyoo na miundombinu mingine muhimu.