Shirika lisilo la kiserikali la DSW Tanzania linalojishughulisha na afya na maendeleo ya vijana kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wametoa mafunzo ya kuimarisha mifumo ya kuzuia ukatili wa kijinsia mkoani Mbeya.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanatolewa katika kikao kazi kinachofanyika kwenye ukumbi wa Meya uliopo jengo la Halmashauri ya Jiji la Mbeya tarehe 24-25 Aprili,2024.
Mkurugenzi wa shirika la DSW Tanzania Bw. Peter Luwaga amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha mifumo ya kuzuia ukatili kwenye nyanja zote kwa watoto na vijana na kujadiliana kuhusu suala zima la ukatili, ulinzi na usalama wa watoto mtandaoni, ndani na nje ya shule.
Bw.Luwaga amesema kuimarisha mifumo ya kuzuia ukatili kwa vijana ambao ni kundi kubwa itawawezesha kuendesha uchumi na kuleta maendeleo kwa taifa na kuepukana na changamoto nyingi zinazosababishwa na mambo mengi ambayo ni pamoja na changamoto za ajira, afya hivyo stadi za maisha ni muhimu ili kuepuka na kujiepusha na vitendo viovu kama madawa ya kulevya.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw.Victor Rugalabamu amesema miongoni mwa sababu zinazochangia ukatili ni pamoja na mila na desturi potofu, malezi duni, migogoro katika familia, umaskini wa kipato na imani za kishirikina.
Aidha Afisa mwandamizi huyo ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Watoto Duniani ( Unicef) mwaka 2015, Asilimia Sitini (60%) ya ukatili ulikuwa unafanyika majumbani, hivyo Serikali na Shirika la DSW Tanzania likaanzisha dawati la mifumo ya ulinzi na usalama kwa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili.
Ameongeza kuwa mifumo hiyo itasaidia kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ukatili kwa vijana na watoto.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Bi.Matilda Luvanda ameeleza kuwa kuimarishwa kwa mifumo hiyo kutasaidia zoezi la utoaji taarifa kwa wanafunzi wahanga wa matukio ya ukatili yanayofanyika shuleni na majumbani.
Katika kikao hicho shirika la DSW Tanzania limetoa vifaa vya michezo kwenye baadhi ya shule ambavyo ni jezi na mipira sambamba na runinga zitakazokuwa zikitumika kufundishia mapambano dhidi ya ukatili.
Naye mwanafunzi Hance Raymond Mveka amewashukuru wawezeshaji wa shirika la DSW Tanzania kwa vifaa hivyo ambapo runinga zitatumika kujifunza mbinu za kupambana na ukatili huku akieleza kuwa vifaa vya michezo vitawasaidia kuimarisha vipaji vyao vitakavyowawezesha kupata ajira na kujiongezea kipato.
Kikao kazi hicho kinachofanyika mkoani Mbeya kinahudhuriwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Elimu Sekondari, Waendesha Mashitaka, Wawakilishi wa Mahakama, Wasimamizi wa Masuala ya Ulinzi na Usalama, Wawakilishi wa Dawati la Jinsia na Wakuu wa Shule katika Halmashauri tatu za wilaya za Rungwe, Mbeya na Jiji na baadhi ya wanafunzi ambao ni walengwa wakuu. Mikoa mingine itakayonufaika na mpango huu ni pamoja na Songwe, Kilimanjaro na Arusha.