Mkurugenzi wa Miradi – Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bw. John Steven.
………………….
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika kipindi cha awamu ya pili ya utekelezaji iliyoanza mwaka 2020 umefanikiwa kutoa ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 800 Tanzania bara na visiwani na kufanikiwa kuimarisha kiuchumi wa kaya maskini katika kuhakikisha wanapiga hatua katika maendeleo.
Akizungumza leo Aprili 24, 2024 katika Maonesho ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Miradi – Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bw. John Steven, amesema kuwa walengwa wamefanikiwa kuimarika kiuchumi na kuweza kusaidia familia zao ikiwemo kusomesha na kujenga nyumba.
Bw. Steven amesema kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao kwa sasa wametoa ruzuku shilingi bilioni 17.5 kwa halmashauri mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani katika maeneo ya utekelezaji 35, huku maeneo 18 yakiwa katika mchakato wa utekelezaji.
“Miongoni mwa majukumu yetu ni kuunda vikundi ili wanachana waweze kujitegemea, pia kutoa ruzuku ya uzalishaji ambapo ni eneo jipya; TASAF imeanza kutekeleza kwa awamu ya pili ya Mpango Kunusuru Kaya za Walengwa“, amesema Bw. Steven.
Amefafanua kuwa wanachama wanaofanya vizuri katika vikundi wanapewa fedha wastani wa shilingi 350,000 kwa ajili ya kuongeza mtaji katika biashara ambazo tayari wameanza kufanya“, amesema Bw. Steven.
Amesema kuwa kazi yao ni kuinua kaya maskini na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kama inavyoonekana katika maonesho ambapo vikundi mbalimbali kutoka bara na visiwani wameshiriki kuonesha shughuli zao za kilimo pamoja na biashara.
Bw. Steven amesema kuwa TASAF ni mpango unaotekelezwa Tanzania bara na Visiwani na sasa wapo katika awamu ya pili ya utekelezaji wa Kunusuru Zaya za Walengwa.
Amesema kuwa wapo katika maeneo ya utekelezaji 186 ambazo ni halmashauri zote za Tanzania bara na visiwani ikiwa na kazi kubwa ya kutoa ruzuku pamoja na kutoa ajira za muda, kuimarisha miundombinu, idara mbalimbali wanazoshirikiana nazo pamoja na kukuza uchumi wa kaya kupitia vikundi vya kuweka na kukopeshana.
Ameeleza kuwa Tanzania bara na visiwani kuna vikundi 56,000 kati ya hivyo vikundi 49,000 sawa na asilimia 88 tayari vimeingizwa katika mfumo, huku vingine vikiwa katika utaratibu wa kuingizwa katika mfumo huo.
Amesema kuawa vikundi 49,000 ambavyo vipo katika mfumo vinatoa fursa ya muda wowote kuweza kupata taarifa zao za utendaji.
Bw. Steven amesema kuwa kupitia vikundi 56,000 mpaka sasa kuna wanachama 778,000 kati ya hao wanaume ni 115,000 huku wanawake wakiwa 663,000.
TASAF inashirikia katika Maonesho ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam yakiwa na kauli mbiu : Tumeshikamana, tumeimarika kwa maendeleo ya Taifa.