Home LOCAL POLISI, NSSF WAKAMATA WATUHUMIWA 30 KWA KUJIPATIA MALIPO KWA NJIA YA UDANGANYIFU...

POLISI, NSSF WAKAMATA WATUHUMIWA 30 KWA KUJIPATIA MALIPO KWA NJIA YA UDANGANYIFU KUTOKA NSSF

 

*Yumo Mwalimu wa Shule ya Msingi, Ofisa wa Benki

 

*SACP Muliro atoa onyo kali, asema hakuna atakayebaki salama
Na MWANDISHI WETU
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na maofisa kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wamefanikiwa kuwakamata watu 30 wanaotuhumiwa kughushi nyaraka mbalimbali zinazohusiana na mafao ya NSSF kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Mwandamizi wa Polisi, SACP Jumanne Muliro, amewataja baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni Mwalimu wa Shule ya Msingi, Docress Kahwa (35), mkazi wa Mbezi Dar es Salaam.
SACP Muliro alisema mtuhumiwa huyo alikuwa na Barnabas Bonivencha na wenzake 11 wa kampuni binafsi ya ulinzi ya G4S ambao kwa nyakatai tofauti waliwasilisha taarifa za uongo za kuachishwa kazi kwa lengo la kupata mafao wakati bado wapo kazini, hati za matibabu ya uongo na wengine walikuwa na hati mbalimbali za NSSF wakiwa na malengo ya kujipatia fedha za mafao.
Alisema watuhumiwa wengine waliokamatwa ni pamoja na Regori Rweikiza (44), mkazi wa Goba na Coroline Mushi (37), mkazi wa Upanga ambaye ni mtumishi wa Benki ya Stanbic, ambao walighushi baadhi ya nyaraka na taarifa za hospitali za ugonjwa, kwa malengo ya kupata mafao yanayohusiana na matibabu.
SACP Muliro alisema watuhumiwa wengine ni Michael Mpogolo (38) Sabato Thomas wote wakazi wa Madale Mivumoni, ambao wanatuhumiwa kughushi nyaraka mbalimbali za wafanyakazi, pia walighushi nyaraka za watu ambao wameshafariki waliofahamika kwa majina ya Cevas Tesha na Condas Show waliokuwa wakifanya kazi kwenye mgodi wa Geita.
“Walighushi nyaraka za marehemu wakajifanya wapo hai, wakijifanya wanafuatilia mafao ya watu ambao walikwishafariki dunia jambo ambalo ni kinyume cha sheria za NSSF,” alisema SACP Muliro.
Alisema watuhumiwa hao ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakighushi nyaraka mbalimbali zikiwemo za matibabu, za kujifanya wamefukuzwa kazi wakati wapo kazini na zinazohusina na mafao mbalimbali ambayo yanalipwa na NSSF, wamehojiwa kwa kina na baadhi ya vielelezo ambavyo ni sehemu ya ushahidi vimepatikana na watafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa watuhumiwa hao na watu wengine kuachana na fikra za kujihusisha na mambo ya kughushi nyaraka mbalimbali na kupanga mipango ya kuyaibia Mashirika haya zikiwemo mamlaka nyingine za kisheria, kwani kufanya hivyo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wataalamu walioko kwenye mamlaka hizo hawatasita kumfuatilia mtu mmoja mmoja au kikundi na kuhakikisha wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema SACP Muliro.
Alisema watuhumiwa wote hao wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here