Home LOCAL KILELE MAADHIMISHO MIAKA 60 YA MUUNGANO KUFANYIKA UWAJANJA WA UHURU DAR ES...

KILELE MAADHIMISHO MIAKA 60 YA MUUNGANO KUFANYIKA UWAJANJA WA UHURU DAR ES SALAAM

Na: Georgina Misama, Maelezo

Tanzania itafikisha miaka 60 ya muungano ifikapo tarehe 26 Aprili, 2024, sherehe za kilele cha maadhimisho zitafanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Aidha, uzinduzi wa sherehe hizi utafanyika tarehe 14 Aprili katika Uwanja wa Amani mjini Zanzibar ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumzia ratiba ya maadhimisho hayo leo Aprili 12, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi amesema, tarehe 19 Aprili, 2024 kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam kutafanyika maonesho ya biashara ambapo Mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Abdullah.

Vile vile, amesema ifikapo tarehe 22 Aprili, 2024 kutafanyika maombi na dua kuliombea taifa katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ambapo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango. Aidha, tarehe 23 Aprili kutakuwa na uzinduzi wa kitabu cha historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo imefikisha miaka 60, uzinduzi huo utafanyikia Ikulu, Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kuanzia tarehe 15 Aprili hadi tarehe 31 Mei, 2024, miradi mbalimbali ya maendeleo itakuwa ikizinduliwa na viongozi mbalimbali nchini kote, ambapo tarehe 25 Aprili kutakuwa na tamasha la miaka 60 ya muungano Iitakalofanyika katika wilaya zote nchi nzima lakini kwa Dar es Salaam litafanyikia katika uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe. Mgeni rasmi katika tamasha hilo atakuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko,” amesema Matinyi.

Ameongeza kwamba, awali tarehe 8 Aprili, 2024 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alizindua kauli mbiu inayosema; MIAKA 60 YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA; TUMESHIKAMANA NA TUMEIMARIKA, KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU na nembo inayotakiwa kutumika katika nyaraka za serikali, matangazo, mialiko, mapambo na pia kutumika kwenye Vituo vya televisheni vya umma na binafsi katika kipindi hiki cha kusherehekea miaka 60 ya muungano aidha, vyombo vya habari vinaombwa kutia hamasa katika shamrashamra hizi za Tanzania kufikisha miaka 60 ya muungano.

Previous articleSERIKALI KUANZA KUTEKELEZA MRADI BONDE LA MSIMBAZI
Next articleKINANA KUWASHA RORYA, KUANZA ZIARA YA KIKAZI APRIL 14
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here