Home BUSINESS GAVANA TUTUBA ATANGAZA RIBA MPYA YA BENKI KUU

GAVANA TUTUBA ATANGAZA RIBA MPYA YA BENKI KUU

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, (BoT), Emmanuel Tutuba, akizungumza alipokuwa akitangaza Riba mpya ya Benki hiyo, leo April 4,2024, Jijini Dar es Salaam.

DAR ES SALAAM.

Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania, (MPC) imetangaza Riba mpya ya Benki hiyo ya robo ya pili ya mwaka kutoka asilimia 5.5 hadi 6 itayoanza kutumika katika kipindi cha mwezi April hadi June, mwaka huu.

Akizungumza leo Aprili 4 Jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, (BoT), Emmanuel Tutuba,  amesema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Aprili 3,2024, na umezingatia tathmini ya mwelekeo wa uchumi iiliyofanyika mwezi Machi, mwaka huu.

Amesema kuwa Kamati hiyo imeona umuhimu wa kuongeza Kiwango hicho cha Riba itakayokuwa na wigo wa asilimia mbili juu na chini, ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei siku zijazo, kutokana na athari za mwenendo wa uchumi wa Dunia.

“Mfumuko wa bei umeendelea kupungua, sambamba na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha, bei za bidhaa katika soko la Dunia imebaki tulivu. Mathalani, bei ya mafuta ghafi ilikuwa wastani wa Dola za marekani 80 kwa pipa, wakati bei ya dhahabu imeendelea kubaki juu, ikiuzwa kwa wastani wa dola za Marekani 2,071 kwa wakia moja,” amesema.

Aidha, Gavana Tutuba amesema hali hiyo inatarajiwa kuendelea katika kipindi kijacho cha mwaka huo na matarajio hayo yanaweza kuathiriwa na uamuzi wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi (OPEC+) kuhusu kiwango cha uzalishaji pamoja na migogoro ya kisiasa inayoendelea.

MWENENDO WA UCHUMI

Kuhusu mwenendo wa uchumi wa nchini, Gavana Tutuba amesema Kamati imeridhishwa na kuendelea kwa uchumi, licha ya changamoto zilizotokana na mtikisiko katika uchumi wa Dunia, na kwamba hali hiyo ya kuimarika kwa uchumi inatarajiwa kuendelea katika siku zijazo, hususani robo ya pili ya mwaka huu.

MAENEO YALIYOFANYIWA TATHMINI

Gavana Tutuba ametaja maeneo mahususi ya mwenendo wa uchumi yaliyofanyiwa tathmini na Kamati kuwa ni ukuaji wa uchumi unakadiriwa kuongezeka kufikia asilimia 5.1 kwa mwaka 2023, kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022.

Ameeleza kuwa ukuaji wa uchumi unakadiriwa kufikia asilimia 5.1 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024.

“Mwenendo huu unatokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali hususani katika ujenzi wa miundombinu unaolenga kuongeza uwekezaji kwa sekta binafsi.

“Vilevile, sekta binafsi imeendelea kuchangia katika kuimarika kwa uchumi kutokana na maboresho yanayoendelea katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Hali hii inadhihirika kutokana na kuendelea kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi na uwekezaji kutoka nje ya nchi,” ameeleza.

Akizungumzia upande wa Zanizabar, Gavana Tutuba amesema mwenendo wa uchumi wa Zanzibar umeendelea kuwa wa kuridhisha, na kwamba umekadiriwa kukua kwa zaidi ya asilimia sita kwa mwaka 2023 kutokana na kuimarika kwa shughuli za uchumi, hususani utalii.

“Mwenendo huu wa kuridhisha wa ukuaji wa uchumi nchini unatarajiwa kuendelea katika kipindi kijacho cha mwaka 2024. Hali hii inatokana na maboresho yanayoendelea katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, mvua za kutosha katika maeneo mengi nchini na kuendelea kuimarika kwa uchumi wa dunia,” amesema.

Pia, mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu, kwa wastani wa asilimia 3.0 kwa robo ya kwanza ya mwaka huu, kiwango hicho kilikuwa ndani ya lengo la nchi la mfumuko wa bei usiozidi asilimia tano na vigezo vya kikanda kwa jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama.

Hali hiyo inatokana na utekelezaji wa sera madhubuti ya fedha na uwepo wa chakula cha kutosha nchini.

Previous articleRAIS SAMIA  AZINDUA TUME YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI JIJINI DAR
Next articleMONGELLA AKABIDHIWA ‘MIKOBA’ RASMI YA NAIBU KATIBU MKUU CCM BARA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here