Home BUSINESS TFS YABAINISHA MAFANIKIO YAO MIAKA MITATU YA Dkt. SAMIA

TFS YABAINISHA MAFANIKIO YAO MIAKA MITATU YA Dkt. SAMIA

Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa Misitu Tanzania, Professa Dos Santos Silayo akizungumza alipokuwa akitoa mada katika mkutano wa Wahariri na waandishi wa Habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, leo Machi 18,2024 Jijini Dar es Salaam.

Afisa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabatho Kosuri, akizungumza alipokuwa akiongoza mjadala na maswali ya Wahariri na waandishi wa Habari katika mkutano huo.

Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa hilo, Salim Said Salim, akizungumza kwaniaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Deodaus Balile, katika mkutano huo.

(PICHA NA: Hughes Dugilo)

Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.

Wakala wa misitu Tanzania TFS imeelezea mafanikio walioyapata katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ambapo wamefanikiwa kushughulikia migogoro 423 kati ya 438 iliyokuwepo kati ya Hifadhi na jamii.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa Misitu Tanzania, Professa Dos Santos Silayo wakati alipokuwa akitoa mada katika mkutano wa Wahariri na waandishi wa Habari  katika mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kuelezea mafanikio waliyopata katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita, ya Dkt. Samia.

Prof. Silayo amesema katika utatuzi huo wa migogoro, jumla ya hekta 296,881 za maeneo ya hifadhi zilitolewa kwaajili ya makazi,  kilimo na ufugaji huku wakitoa elimu ya uhifadhi na usimamizi wa misitu na kuimarisha mipaka kwa kuweka vigingi na mabango, ili kuzuia uvamizi.

“Niiombe jamii iwe nasi katika safari hii ya uhifadhi wa rasilimali za misitu kwaajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vya baadae, tujiepushe kuchoma moto misitu na uvunaji haramu.”

Aidha amesema katika jitihada za kukabiliana na majanga ya moto kwenye hifadhi za misitu, Wakala wamesafisha mipaka na njia za moto zenye urefu wa kilomita 13,426 huku wananchi zaidi ya 29,685 kutoka vijiji 749 vinavyozunguka misitu 120 wakipatiwa elimu ya athari za moto na mbinu za kukabiliana nao.

“Kutokana na juhudi hizo, matukio ya moto yalipungua kwa asilimia 11 kwa mfano, eneo la msahamba ya miti lililoharibiwa kwa moto mwaka 2023/24 ilikua hekari 400 ukilinganisha na 3, 200 kwa mwaka uliotangulia” Alisema Silayo.

Akizungumzia  Utalii, ikolojia na utamaduni, Prof. Silayo amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa juhudi zake za makusudi alizozichukua kuandaa filamu ya Tanzania the royal Tour ambayo imepelekea kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea vituo vya utalii na ikolojia, na kuongeza mapato ya nchi.

“Juhudi zilizofanyika zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea vituo vya utalii ikolojia kutoka 59,606 mwaka 2021/2021 hadi 242,824 mwaka 2022/2023 na mapato katika kipindi hicho yaliyoongezeka kutoka shilingi 154,965,050 hadi kufikia wastani wa Shilingi 1,5018,940,965.” Alisema

Katika wasilisho lake pia amezungumzia ufugaji nyuki, na kusema kuwa uzalishaji wa mazao ya nyuki nchini umeongezeka hadi kufikia wastani wa tani 32,691 kutoka tani 31,179 sawa na ongezeko la asilimia 5, na kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Tanzania imeuza jumla ya tani elfu 5.6 za asali yenye thamani ya Dolla za Marekani milioni 40 nje ya nchi.

Prof .Silayo ameitaja mipango yao ya baadae ikiwa ni pamoja na kuokoa na kuzuia uharibifu wa misitu kwa kiasi cha
hekta 5.2million kufikia mwaka 2030, sambamba na kuongeza upatikanaji wa malighafi ya viwanda vya misitu kwa kupanda miti na kuongeza mashamba ya miti, kuimarisha utalii ikologia na utalii wa nyuki. Lakini pia Kuongeza mapato ya taasisi kwa kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na fursa za biashara ya kaboni.

Previous articleSOMA MAGAZETI YA LEO JUMANNE MACHI 19-2024
Next articleWAGOMBEA 127 WA UDIWANI KUTOKA VYAMA 18 KUPIGIWA KURA KESHO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here