Tanzania na Pakistan zimeahidi kuendelea kushirikiana kuimarisha zaidi sekta za biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili.
Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvastory Mbilinyi alipokutana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Bw. Shehryar Akbar Khan katika majadiliano ya Kidiplomasia kati ya Tanzania na Pakistan kwa lengo la kuimarisha, kukuza na kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kipaumbele.
Bw. Mbilinyi amesema Pakistan ni miongoni mwa nchi za Asia ambazo zina majadiliano ya kidiplomasia na Tanzania.
Amesema chimbuko la majadaliano hayo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Pakistan.
Akizungumza katika mkutano uliokutanisha pande hizo mbili katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Bw. Mbilinyi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita zaidi katika kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji nchini hivyo wafanyabiashara kutoka Pakistan wasisite kuwekeza Tanzania kwani ni salama.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Bw. Shehryar Akbar Khan amesema Pakistan na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali wakati wote.
“Nchi zetu zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali, ila kwa sasa tunaona ni vyema zaidi tukaimarisha zaidi sekta ya biashara na uwekezaji kwani kila nchi inahitaji biashara na uwekezaji,” alisema Bw. Khan na kuongeza kuwa Pakistan imekusudia kushirikiana na Tanzania katika sekta ya uchumi wa buluu.
Katika mazungumzo hayo pande zote mbili zimeahidi kuimarisha ushirikiano katia sekta za elimu, afya, ulinzi, kilimo, nishati uchumi wa buluu na usafirishaji.