Home LOCAL WATENDAJI WATAKIWA KUFANYA UCHAGUZI KWA UFANISI

WATENDAJI WATAKIWA KUFANYA UCHAGUZI KWA UFANISI

Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Rufaa (Mstaafu) Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa watendaji wa Uchaguzi ambao wanakwenda kusimamia uchaguzi mdogo katika Kata 23 za Tanzania Bara yaliyofanyika kwa siku tatu mkoani Morogoro. Uchaguzi unataraji kufanyika Machi 20,2024. (Picha na NEC).

Sehemu ya washiriki wa mafunzo kwa watendaji wa Uchaguzi mdogo wa udiwani kwa Kata 23 za Tanzania bara yaliyofanyika mkoani Morogoro kwa siku tatu. Uchaguzi unataraji kufanyika Machi 20,2024.(Picha na NEC).

Na Mwandishi wetu, Morogoro

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewakumbusha watendaji wa uchaguzi kwenye uchaguzi mdogo wa kata 23 za Tanzania Bara kukamilisha maandalizi muhimu kwa wakati ili kuwezesha uchaguzi huo kufanyika kwa ufanisi.

Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Rufaa (Mstaafu) Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk leo tarehe 22 Machi, 2024 wakati akifunga mafunzo kwa watendaji hoa yalifanyika mkoani Morogoro.

Uchaguzi huo utafanyika tarehe 20 Machi, 2024 ambapo fomu za uteuzi zitatolewa kuanzia tarehe 27 Februari, 2024 hadi tarehe 04 Machi, 2024, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 04 Machi, 2024 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 05 hadi 19 Machi, 2024.

“Mnatakiwa kukamilisha mambo yote muhimu yanayotakiwa kwenye mchakato wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kubandika matangazo na mabango mbalimbali ya kisheria kuhusiana na uchaguzi kwa mujibu wa maelekezo,” amesema Jaji Mbarouk.

 Aliwakumbusha watendaji hao kuwa wapo wadau mbalimbali wa uchaguzi kama vile vyama vya siasa, wananchi na watazamaji ambao wanafuatilia uendeshwaji wa uchaguzi na kiwango cha uzingatiwaji wa sheria zinazohusiana na uchaguzi. Hivyo, ni muhimu wakatekeleza kila hatua na kila jambo linalotakiwa kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi.

“Jukumu lililopo mbele yetu ni kubwa na muhimu na linahitaji umakini, na kujitoa, na hasa baada ya kupatiwa mafunzo haya, mtatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na weledi mkizingatia ratiba ya utekelezaji ili kufanikisha uchaguzi wa tarehe 20 Machi, 2024,” Jaji Mbarouk amewaambia watendaji hao.

 Amesisitiza juu ya umuhimu wa watendaji hao kutenga sehemu ya muda wao kusoma Katiba, Sheria na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume ili yawaongoze katika kusimamia uchaguzi utakaokuwa huru na wa haki.

Kata zitakazofanya uchaguzi huo mdogo ni Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Fukayosi    (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).

Nyingine ni  Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Mshikamano (Halmashauri ya Wilaya ya Musoma), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Nkokwa (Halmashauri ya Wilaya ya Kyela), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu) Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).

Mwisho.

Previous articleCCM ZANZIBAR KUENDELEZA USHIRIKIANO NA FRELIMO
Next articleRAIS SAMIA AIPONGEZA KUWAIT KUADHIMISHA MIAKA 63 YA TAIFA HILO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here