Home LOCAL VIUMBEPORI BAHARI HATARINI KUTOWEKA 

VIUMBEPORI BAHARI HATARINI KUTOWEKA 

Na Selemani Msuya

KUKOSEKANA juhudi za pamoja za Serikali, wadau wa uhifadhi na wananchi kukabiliana na uvunaji haramu wa viumbepori na bahari baada ya miaka mitano kutasababisha viumbe hao kutoweka.

Taarifa zinadai kuwa uvunaji haramu wa viumbe hao kwa mwaka huchangia hasara ya zaidi ya dola za Marekani bilioni saba hadi 23 na kutoa ishara mbaya kwa siku zijazo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki na wanahabari walioshiriki mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), Mkuu wa Kitengo cha Sera na Usimamizi wa Maliasili kutoka Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Allen Mgaza amesema kasi ya uwindaji inaongezeka siku hadi siku, hivyo kushauri nguvu zaidi ya udhibiti iongezwe.

Amesema kwa miaka ya karibuni, wameshuhudia ukamataji wa magamba ya kakakuona na viumbe wengine, hali inayohitaji nguvu ya makundi yote ili kukabiliana nayo.

Amesema biashara hiyo inashika namba nne kati ya biashara haramu duniani ikitanguliwa na ya usafirishaji dawa za kulevya, binadamu na bidhaa bandia.

Mgaza amesema kwa sasa Dunia inapitia wakati mgumu wa kukabiliana na uvunaji wa kakakuona na majongoo bahari kinyume na utaratibu, hivyo ni jukumu la kila mdau kushiriki kukabiliana na hali hiyo.

Amesema hivi karibuni tani sita za magamba ya kakakuona zilikamatwa Malaysia jambo ambalo ni ushahidi tosha kuwa hali ni mbaya.

Mgaza amesema ukamataji huo, hauko Malaysia pekee bali hata Tanzania baadhi ya watu wamekamatwa na magamba hayo wakisafirisha.

Amesema pamoja na changamoto ya uwindaji haramu wa wanyama hao, Tanzania imesaini mkataba wa CITES wa kimataifa unaodhibiti biashara ya viumbe walio hatarini kutoweka na kuboresha sheria ili kuakisi makubaliano na mikataba ya kimataifa.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo, ni vema elimu ikatolewa, huku kasi ya usimamizi wa sheria ikiongezeka, ili kuchukua hatua kwa yeyote atakayekwenda kinyume.

Aidha, Mgaza amesema tembo ni viumbepori walioko hatarini kutoweka kutokana na kasi kubwa ya uvunaji, ikichangiwa na soko kubwa katika nchi za Asia.

“Si lazima awe mnyama mzima, bali hata sehemu za miili yao kama vile ngozi, magamba, kucha, nyama, pembe, meno au mifupa yao, vyote hivyo vinapaswa kudhibitiwa, kwani biashara ikiendelea viumbe hao watatoweka,” amesema.

Mkufunzi na mwandishi wa habari mkongwe, Pili Mtambalike amewataka wanahabari kutumia kalamu zao kuandika bahari zinazotoa matokeo chanya, ili kuhakikisha viumbe walio hatarini kutoweka, wanaokolewa.

“Tumepata mafunzo mazuri, ni wakati mwafaka kuandika habari za kina kuhusu changamoto hii ya viumbepori na bahari kutoweka kwa siku zijazo, habari hizo zitaleta mabadiliko chanya,” amesema.

Previous articleWAZIRI KAIRUKI AZINDUA VITENDEA KAZI VYA DORIA MISITUNI VYENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 6
Next articleWASIMAMIZI WA UCHAGUZI WAASWA KUFUATA NA KUZINGATIA SHERIA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here