Wahadhiri na Wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wamehamasishwa kuchagua maeneo ya kubobea katika taaluma ya kisayansi ili waweze kuandika maandiko mbalimbali ya maombi ya hataza na Miliki Ubunifu.
Hamasa hiyo zimetolewa na Afisa Sheria kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Andrew Malesi wakati akitoa elimu ya Miliki Ubunifu chuoni hapo tarehe 5 Februari , 2024 jijini Dar es Salaam.
Bw. Malesi ameshauri pia ni vyema wanafunzi wa kada mbalimbali wakaona umuhimu wa kushiriki mafunzo kama haya kwa sababu maisha ya binadamu ya kila siku yanazungukwa na kazi za Miliki Ubunifu ambazo kimsingi ni moja ya vyanzo vya mapato kwa wabunifu na watumiaji wa kazi za Miliki Ubunifu.
“Mtu akiwa na uelewa wa Miliki Ubunifu atajua namna bora ya kulinda ubunifu wake na namna bora ya kuingiza ubunifu wake kwenye soko la ndani na nje,” amefafanua Bw. Malesi.
Naye Afisa Usajili kutoka BRELA Bw. Stanislaus Kigosi amesema kuwa TIA inafanya tafiti mbalimbali ambazo matokeo yake yanaweza kufanyiwa mchakato wa kuwa bidhaa au namna za kutengeneza vitu mbalimbali hivyo, wakilinda vumbuzi hizo zitakuwa na manufaa kwa mbunifu, chuo na jamii kwa ujumla.
Ameongeza kwa kufafanua kuwa haki za Miliki Ubunifu ikiwemo Hataza na Alama za Biashara na Huduma zimekuwa na thamani ulimwenguni hivyo Bunifu wanazo zianzisha au wanazozibuni wahakikishe wanazisajili BRELA ili zilindwe na ziweze kunufaisha na kusaidia jamii.
Aidha, Msaidizi wa Usajili wa BRELA Bw. Benedickson Byamanyilwowa, amesema kuwa Hataza zinazobuniwa katika Miliki Ubunifu zote zinazosimamiwa na kulindwa na BRELA, zinafanyika kwa njia ya mtandao ambao unapatikana katika tovuti ya www.brela.go.tz lengo likiwa ni kuokoa muda na kupunguza gharama kwa wadau.
Awali akitoa neno la ukaribisho Mkuu wa Idara ya Ukuzaji na Uendelezaji wa Wanafunzi Kitaaluma na Kitaalam, Bw. Imani Matonya amewapongeza BRELA kwa kuandaa mafunzo hayo ya Miliki Ubunifu na kufika katika Chuo hicho ambacho kinafundisha taaluma mbalimbali ikiwemo ya Miliki Ubunifu na Elimu ya Biashara.
Pia amewataka BRELA kuendelea kufika katika Chuo hicho, pale wanapopewa mialiko na kutoa mafunzo kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA.
Kwa upande wake Bi. Lilian Rugaitika, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Masoko , TIA amewashukuru BRELA kwa mafunzo ya Miliki Ubunifu kwa wanafunzi na watumishi kwani Chuo Kikuu ni Taasisi inayotoa elimu kwa nadharia na vitendo, hivyo ujio wa BRELA unakamilisha dhana ya kutoa elimu kwa vitendo.