Home BUSINESS TANZANIA YATOA MSIMAMO WAKE  WTO

TANZANIA YATOA MSIMAMO WAKE  WTO


Tanzania ikiwa ni mmoja wa waanzilishi wa Shirika la Biashara Dumiani (WTO) inaunga mkono mfumo wa biashara unaotegemea sheria ambazo zinatoa ulinzi na fursa kwa Nchi wanachama wote haswa Nchi zinazoendelea katika kuhakikisha maendeleo endelevu duniani yanapatikana

Vilevile, Tanzania inaunga mkono maboresho ya WTO yanayohakikisha maslahi ya usawa ya Wanachama na haswa kuunga mkono nchi zinazoendelea na nchi zisizo na bandari (LDCs) kufikia lengo pana la ushirikishwaji na kukuza maendeleo endelevu kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Marrakesh kuanzisha WTO.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah Februari 26, 2024 wakati akitoa msimamo wa Tanzania katika Mkutano wa 13 wa Mawaziri wa Biashara (M13) unaoendelea kufanyika kuanzia tarehe 26 hadi 29/02/ 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa ADNEC, Abudhabi katika Falme za Kiarab.

Aidha, amebainisha kuwa Tanzania inaendelea kusisitiza kuwa matokeo ya mafanikio ya maboresho hayo yanapaswa kuwa sawa, na kuzingatia mahitaji tofauti ya wanachama kulingana na tofauti zao za uchumi na maendeleo pamoja na kulenga kurekebisha baadhi ya sheria za biashara ambazo kwa namna fulani zimesababisha kufa kwa viwanda katika baadhi ya nchi wanachama.

Kwa upande wa Mkataba wa Ruzuku kwa wavuvi , Dkt Abdallah amesema Tanzania itahakikisha kuwa rasilimali za uvuvi zinavunwa kwa njia endelevu na rafiki kwa kuwa kwa Nchi nyingi zinazoendelea na Nchi za LDCs, sekta ya uvuvi ndiyo nguzo ya ajira kwa jamii zinazozunguka maeneo ya maji, hivyo kuwa chanzo cha mapato na chakula kwa maisha ya vijijini na mijini na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi wa nchi hivyo ni muhimu kuhakikisha mkataba huo unajumuisha matibabu maalum na tofauti yanayofaa ikiwa ni pamoja na misaada ya kiufundi na kujenga uwezo kwa nchi hizo zinazoendelea.

“Uvuvi ni shughuli muhimu ya kiuchumi kwa Tanzania na ina ukanda wa pwani wenye urefu wa kilomita 1424 na Eneo la Kiuchumi la Pekee la kilomita za mraba 223,000 ambapo Sekta ya uvuvi inawaajiri wavuvi wapatao 200,000 wa moja kwa moja na jumla ya samaki wanaovuliwa ni tani takriban 415,000 kwa mwaka” Alibainisha Dkt Abdallah.

Aidha katika hatua nyingine, Dkt. Abdallah amesisitiza hatua za kuhakikisha usalama wa chakula, zinakuwa jumuishi katika kushughulikia mahitaji katika mnyororo wa thamani, ikiwa ni pamoja na teknolojia mpya zinazohusiana na uzalishaji wa vyakula vya msingi, usindikaji, uhifadhi na uuzaji wa bidhaa za kilimo ambazo kwa upande wake zitaathiri vyema uzalishaji, ushindani na maisha ya wakulima na jamii za vijijini katika nchi zinazoendelea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here