TMDA
Home BUSINESS TANZANIA YAJIPANGA KUWA GHALA LA CHAKULA DUNIANI

TANZANIA YAJIPANGA KUWA GHALA LA CHAKULA DUNIANI

Na Farida Ramadhani na Joseph Mahumi, (WF) Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ametoa wito kwa Wadau wa Maendeleo kushirikiana na Tanzania kupanga mikakati itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kwa kuboresha mifumo yake ya uzalishaji na kuiwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula na kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula duniani.

Dkt. Mwamba ametoa wito huo jijini Dar es Salam wakati akifungua Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo ngazi ya Wataalam uliowashirikisha wadau wa maendeleo wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, Asasi zisizo za Kiserikali (AZAKI), na Viongozi waandamizi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kuwa dunia imepitia kipindi cha ukosefu mkubwa wa uhakika wa chakula kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na umaskini, mabadiliko ya hali ya hewa na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa katika baadhi ya nchi duniani.

“Tanzania ina uwezo wa kuwa kitovu cha uzalishaji na ghala la chakula katika eneo la Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa ujumla ingawa uwezo huu bado haujatumika ipasavyo”,alibainisha Dkt. Mwamba.

Dkt. Mwamba ambaye ni Mwenyekiti wa Mkutano huo alisema Serikali ina miradi mingi ya kubadilisha Sekta ya Kilimo, kwa kuanzia na Ajenda 10/30 kupitia Mpango wa Vijana wa Kujenga Kesho Bora (BBT) ambayo inalenga kuzalisha ajira zaidi ya milioni 1.5 na sekta hiyo inakadiriwa itachangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa asiliasilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Alisema kuna umuhimu wa Serikali na washirika wa maendeleo kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya upangaji, upatikanaji wa rasilimali na mifumo ya uwekezaji ili kuwezesha ukuaji wa maendeleo ya uchumi jumuishi wa Tanzania.

Aidha, Dkt. Mwamba alisema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa umelenga kujadili kimkakati masuala mtambuka yatakayokuwa na mapendekezo yatakayochagiza utekelezaji wa vipaumbele vilivyoelezwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa awa Miaka Mitano, hususan katika kufikia uchumi jumuishi na wenye ushindani, kuimarisha viwanda na utoaji wa huduma, kuhamasisha uwekezaji na biashara pamoja na kukuza uwezo na ujuzi wa rasilimali watu.

“Kupata maendeleo ya haraka kunategemea zaidi uwezo na ubora wa rasilimali watu. Katika jitihada zetu za kudumisha kubaki na hadhi ya Nchi ya Kipato cha Kati cha Chini na kuendeleza nchi kuelekea kiwango cha juu zaidi cha maendeleo, lazima tuwe na mikakati na kipaumbele cha kukuza na kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu hususan, kukuza vipaji, kuendeleza ujuzi, kujenga mazingira rafiki yanayostawisha ubunifu, ujasiriamali, na kuimarisha upatikanaji wa mali”,alisema Dkt. Mwamba.

Aliongeza kuwa katika tekeleza vipaumbele vya Taifa, suala la ufadhili ni muhimu, hivyo alihimiza juhudi za pamoja katika kutafuta rasilimali zenye masharti nafuu ili nchi kuweza kufikia vipaumbele vilivyokusudiwa.

Aidha, aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa michango mbalimbali wanayoitoa katika kuimarisha uchumi wa nchi ulioathiriwa na migogoro ya kimataifa.

Alisema moja ya njia muhimu ya kutoa misaada kama hiyo ni kwa njia ya Misaada ya Kibajeti (GBS)ambapo wamekuwa wakitoa fedha moja kwa moja kuchangia Bajeti ya Serikali hivyo kuongeza hali ya umiliki, uwajibikaji na kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji wakati wa utekelezaji wa miradi na programu za kimkakati.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi na Mratibu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti mwenza wa Washirika wa Maendeleo Nchini, Bw. Zlatan Milisic aliunga mkono jitihada za Serikali za kujiimarisha katika uzalishaji wa chakula.

Alisema kuwa uimarishaji wa mifumo ya chakula na lishe nchini unahitaji mbinu bora za zinazoendana na hali ya hewa, mabadiliko ya kidijitali, upanuzi wa kimkakati wa uzalishaji wa chakula, uhifadhi na usambazaji, usimamizi wa opotevu wa mazao wakati na baada ya mavuno na usaidizi zaidi kwa wakulima wadogo.

Bw. Milisic alisema kuwa Tanzania itaweza kupata maendeleo ya kijamii na kiuchumi ikiwa itashirikiana na wadau wa maendeleo katika kukuza rasilimali watu, kwa kuwekeza kwa vijana, kutoa fursa kubwa kwa wanawake na wasichana, kupata elimu na afya bora pamoja na kuwawezesha wananchi wote kutambua uwezo wao kikamilifu.

Bw. Milisic alisema wadau wa maendeleo wanaishukuru na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuchukua jitihada mbalimbali katika kuimarisha sekta hiyo ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294 miaka michache iliyopita hadi kufikia shilingi bilioni 954 kwa mwaka ahatua mbayo alisema itaimarisha ukuaji wa uchumi na lishe.

Alisisitiza kuwa kilimo bado ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania, kikichangia takribani asilimia 28 katika Pato la Taifa na kuajiri zaidi ya asilimia 65 ya watu, wengi wao wakiwa wanawake na vijana.

Aidha, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mh. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua kubwa iliyofikiwa ya kufanya mijadala kwa ajili ya kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bw. Raphael Maganga na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Asasi zisizo za Kiserikali (AZAKI), Dkt. Lilian Badi, waliipongeza Serikali kwa mipango mbalimbali inayoendelea ya kuboresha mazingira ya baiashara, kukuza ajira, kupunguza umaskini na kukuza uchumi kwa ujumla.

Waliishauri Serikali iendelee kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kuimarisha usalama wa chakula kupitia sekta za kilimo, afya, miundombinu ya umeme wa uhakika na unaotosheleza pamoja na kuimarisha matumizi ya ubunifu na teknolojia katika kuendesha uchumi wa nchi.


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (katikati) akiongoza Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati wa Ngazi ya Wataalamu kwa Mwaka 2024 kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo wenye kaulimbiu,”Kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050; Kuongeza Kasi ya Uchumi Himilivu na Maendeleo Jumuishi katika Nyakati Zisizotabirika”, umehudhuriwa na Wadau mbalimbali wa Maendeleo kutoka nchi mbalimbali, Asasi zisizo za Kiserikali (AZAKI), pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.


Wadau wa Maendeleo wa makundi mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (Hayupo pichani), wakati akifungua Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati wa Ngazi ya Wataalamu Mwaka 2024 kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo wenye kaulimbiu,”Kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050; Kuongeza Kasi ya Uchumi Himilivu na Maendeleo Jumuishi katika Nyakati Zisizotabirika”, umehudhuriwa na Wadau mbalimbali wa Maendeleo kutoka nchi mbalimbali, Asasi zisizo za Kiserikali (AZAKI), pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Open chat
GREEN WAVES MEDIA
Ahsante kwa kutembeiea TANZANIA YAJIPANGA KUWA GHALA LA CHAKULA DUNIANI