Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella kufuatia vifo vya watu 25 na majeruhi 21 vilivyotokea katika ajali ya gari.
Ajali hiyo imetokea jana saa 11 jioni katika barabara kuu ya Arusha – Namanga Ngaramtoni Kibaoni kata ya Orolieni wilayani Arumeru mkoani humo.
Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo, waliopoteza maisha ni wanawake 10, wanaume 14 pamoja na mtoto 1 wa kike wakiwemo raia wa kigeni kutoka mataifa 7 ya Kenya, Togo, Madagascar, Burkina Faso, Afrika ya Kusini, Nigeria na Marekani. Idadi ya majeruhi ni 21 wakiwemo raia wa kigeni kutoka mataifa ya Nigeria, Ivory Coast, Uswizi, Cameroon, Uingereza, Mali na Hawaii.
SACP Masejo amesema ajali hiyo imehusisha gari la kubeba mizigo la kampuni ya KAYCONSTRUCTION ya Nairobi, Kenya likitokea Namanga kwenda Arusha ambalo liligonga magari matatu.
Chanzo cha ajali ni gari hiyo kupoteza uelekeo na kuyagonga kwa nyuma magari matatu yaliyokuwa yakielekea Arusha ambayo ni daladala aina ya Nissan Caravan yenye kufanya safari zake Arusha mjini kwenda Ngaramtoni na Mercedes Benz Saloon (gari binafsi). Gari nyingine ni Toyota Coaster mali ya shule ya New Vision iliyopo Ngaramtoni Arusha iliyowabeba raia wa kigeni wanaofanya shughuli za kujitolea kwenye shule hiyo.
Rais Samia anawapa pole majeruhi wa ajali hiyo pamoja na wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amin.
Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.