Home BUSINESS NAIBU WAZIRI ATAKA UBUNIFU BODI MPYA NEEC

NAIBU WAZIRI ATAKA UBUNIFU BODI MPYA NEEC

Na: Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga amewataka wajumbe wa Bodi ya Saba ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC) kuwa wabunifu sambamba na kuzingatia uadilifu na uweledi ili kuchochea wananchi kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo chini ya Uenyekiti wa Profesa Aurelia Kamuzora Jijini Dar es Salaam, Waziri Nderiananga amesema Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Na. 16 ya mwaka 2004 imeipa bodi mamlaka ya kusimamia baraza, ili liweze kufikia malengo ya Serikali ikiwemo kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imewaamini hivyo jukumu lenu ni kuonesha mchango stahiki ikiwa ni pamoja na kusimamia utendaji wa baraza.

Naamini kwa umoja wenu na ushirikiano na menejimenti ya NEEC mtaweza kufanikisha hili na kuleta matokeo chanya katika kukuza uchumi wa Taifa,” amesema Waziri Nderiananga.

Amesema mafanikio ya NEEC yanategemea kwa kiasi kikubwa miongozo na utendaji wa bodi, ili kuibua na kubuni mbinu zitakazoweza kutanua wigo wa utoaji huduma za uwezeshaji kwa weledi na kufikia wananchi wengi nchini.

“Bodi hii inatarajiwa kutekeleza majukumu yake kwa kipindi cha miaka mitatu, hivyo ni jukumu la bodi kuhakikisha baraza linafikia malengo na matarajio ya wananchi katika kipindi chote cha utendaji wake” amesisitiza Nderiananga.

Aidha, ameipongenza menejimenti ya NEEC kwa utekeleza na kufikia malengo ya kuundwa kwa baraza hivyo ni imani yake kuwa bodi mpya itapata ushirikiano mkubwa.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa NEEC, Bengi Issa, ameahidi kuwa menejimenti yake kwa kushirikiana na wadau watafanya kazi kwa karibu na bodi, ili kufikia azma ya Serikali ya kukuza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za kiuchumi pamoja na manunuzi ya umma hususa makundi maalum (wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu).

“Sisi kama baraza tutaendelea kuratibu wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusimamia mifuko ya uwezeshaji ambayo mpaka sasa tunayo mifuko 72 ambapo 62 ipo ndani ya Serikali na 10 hipo nje ya Serikali, lakini unairatibu na kuhakikisha tunapata taarifa ya utekelezaji wao,” amesema Issa.

Amesema baraza limejipanga kuendelea kuwajengea uwezo watanzania ikiwa ni pamoja na kuendesha mafunzo nchi nzima yatakayo angazia namna bora ya kutumia mifumo iliyoanzishwa na serikali sambamba na kufanya urasimishaji wa biashara ili ziwe rasmi.

Naye Mjumbe wa Bodi iliyomaliza mda wake, Profesa Lucian Msambichaka alisisitiza bodi mpya kufanya kazi kwa umoja ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia Sera, Sheria na Kanuni.

Mwisho.

Previous articleKAMISHNA MABULA AWATAKA MAOFISA WA TAWA KUIMARISHA SHUGHULI ZA UTALII ILI KUONGEZA MAPATO SERIKALINI.
Next articleRAIS SAMIA KUONGOZA MAZISHI YA LOWASSA FEBR. 17
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here