Home LOCAL MSD YAWATAMBUA NA KUWAPONGEZA WADAU WAKE KANDA YA MBEYA

MSD YAWATAMBUA NA KUWAPONGEZA WADAU WAKE KANDA YA MBEYA

Na MWANDISHI WWTU

BOHARI ya Dawa (MSD) imewatambua na kuwapongeza wadau wake wa Kanda ya Mbeya kwa ushirikiano na umahiri wao katika uboreshaji na upatikanaji wa bidhaa za afya kwenye maeneo yao.

Akizungumza katika mkutano huo wa wadau na MSD, Meneja wa MSD Kanda ya Mbeya, Marco Masala alisema mkutano kazi huo umelenga kuweka mkakati wa pamoja wa kudumu na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya katika mikoa hiyo unaboreshwa na unaimarika.

Akisistiza katika mkutano huo ulioambatana na tukio hilo la utoaji vyeti kwa wateja wote na utambuzi wa wadau waliofanya vizuri kwenye maeneo kadhaa kwa kuwapatia tuzo maalumu kutoka mikoa ya Mbeya, Rukwa, Songwe na Halmashauri ya makete iliyopo mkoani Njombe, Masala alisema lengo la mkutano huo ni kuweka mikakati ya pamoja ya kutekeleza majukumu yao na kutatua changamoto zinapojitokeza kwa pamoja.

Akizungumzia tukio la kuwatambua na kuwapongeza wadau hao mahiri alisema hatua hiyo ilifikiwa kutokana namna wanavyotoa ushirikiano dhabiti katika kufanikisha kazi mbalimbali na MSD.

“Wadau hawa tunaowatambua leo ni pamoja na vituo ambavyo havina madeni ndani ya MSD, vinatumia vyanzo vyao vingine kununua bidhaa za afya kutoka MSD, lakini zaidi wanatimiza wajibu ipasanyo wa kuwezesha usambazaji wa vifaa tiba kwa wakati,” alisema Masala.

Aidha Meneja huyo aliongeza kwamba kwa sasa MSD inaendelea kujipambanua kwa ufanisi wa utoaji wa huduma zake kwa kuzingatia mahitaji halisi kuzunguka kanda yote ya Mbeya hivyo kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu kupata vifaa tiba na dawa.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa aliwaomba wadau kutambua kuwa jukumu kubwa walilo nalo ni kuvisimamia vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo yao ili viweze kukusanya mapato ya kutosha yanayotokana na uchangiaji wa huduma za afya ili viweze kununua bidhaa za afya, sambamba na kusimamia mnyororo wa ugavi wa bidhaa hizo.

“Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuongeza fedha inayotengwa kwa ajili ya bajeti ya kununulia bidhaa za afya ili kuboresha utoaji wa huduma za afya. Hivyo, kila mmoja ana jukumu la kusimamia matumizi sahihi ya bidhaa za afya ili kuleta tija kwa wananchi,” alisema Malisa.

Aidha, Malisa aliwataka wadau hao kuhakikisha wananchi watapata huduma bora zaidi katika vituo vya kutolea huduma za Afya bila manung’uniko na kupitia mkutano huo aliwakumbusha wadau wa MSD kupitia Wizara ya Afya, kufanya maoteo ya bidhaa za afya kwa usahihi na kwa wakati.

Alisema kwa kufanya hivyo itaiwezesha MSD kuwa na takwimu sahihi katika kuagiza kutoka kwa wazalishaji na washitiri hivyo kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya.

Malisa aliwakumbusha wadau hao kusimamia matumizi sahihi ya takwimu za mnyororo wa ugavi ili ziwasaidie kufanya maamuzi sahihi juu ya bidhaa za afya katika maeneo yao.

Meneja Huduma kwa Wateja wa MSD, Dkt. Pamella Sawa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai alisema lengo lingine la kikao kazi hicho ni kupeana maelekezo au kutatua changamoto zilizopo baina ya wadau wao na MSD na kuelimishana namna bora ya kufanya kazi kwa kushirikiana na pale watakapo zibaini watafute njia bora ya kuboresha.

Alisema kikao hicho kinahusisha wadau wa mikoa ya Mbeya, Rukwa, Songwe na Halmashauri ya Makete wanaohudumiwa na MSD wakiwemo viongozi mbalimbali wa sekta ya afya na Serikali.

“Sasa hivi kuna mabadiliko na maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ndani ya MSD na ninyi wateja wetu ni mashahidi hasa katika majukumu yetu kwenye eneo la usambazi kutoka mara nne hadi mara sita ya mzunguko na upatikanaji wa bidhaa za afya unakuja kwa wakati,” alisema Dkt. Sawa.

Kwa upande wake Dkt. Enock Mwambalaswa ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri wa Mji wa Tunduma ambayo imepata cheti cha pongezi na tuzo tatu ambazo Halmashauri hiyo imepata ikiwa ni Halsmashauri pekee iliyopata tuzo zote tatu.

Alisema kuwa pia Halmashauri hiyo imeibuka kidedea kwa kupata tuzo kwa kutumia vyanzo vingine vya mapato tofauti na vyanzo vinavyotolewa na Serikali kama ruzuku kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba.

Dkt. Mwambalaswa alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kwa kutoa kipaumbele kwenye mgawanyo wa mapato ambao unaelekeza halmashauri kutoa msukumo kwa kutenga kila asilimia 50 ya mapato yake na kuyapeleka kwenye huduma za afya.

Halmashauri tatu zilizoibuka kidedea kwa kutumia vyanzo vingine vya fedha mbali ya zile zinazo tolewa na Serikali kwa ajili ya kununua bidhaa za afya ni Mbeya mji, halmashauri ya mji wa Tunduma na Halmashauri Mbeya.

Halmashauri tatu za kwanza ambazo vituo vyake vya afya havina madeni au madeni yake kidogo ni Ileje, halmashauri ya mji Tunduma na Busokelo na zote hizi zimetunukiwa tuzo za umahiri.

Previous articleTANZANIA YAJIPANGA KUWA GHALA LA CHAKULA DUNIANI
Next articleNCHI WANACHAMA WA EAC ZAKUBALIANA KUINGIA JUMUIYA ZA KITANDA NA KIMATAIFA KWA PAMOJA 
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here