*Zapongezwa kwa ushirikishwaji mzuri wa wananchi*
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)imezipongeza Kamati za kushughulikia malalamiko wakati wa utekelezaji wa miradi ya majisafi na usafi wa mazingira kwa kazi kubwa iliyofanyika na inayoendelea kufanyika ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazojitokeza
Akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuwasilisha taarifa ya kazi ya usuluhishi wa malalamiko ya wananchi wakati wa utekelezaji wa miradi, kilichohudhuriwa na wajumbe wa kamati za Ubungo na Kinondoni, Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Modesta Mushi amesema kuwa uwepo wa Kamati zimekuwa msaada mkubwa kwa Taasisi na jamii kwa kusaidia kutoa uelewa kwa wananchi kuhusu lengo la Serikali la kutekeleza miradi hii.
Amesema kuwa ili miradi ya majisafi na usafi wa mazingira iweze kukamilika vizuri, panahitajika kamati kama hizi zinazosaidia kuwajengea uelewa wananchi juu ya hatua za utekelezaji wa mradi pamoja na ushirikishwaji wa wananchi kwenye utekelezaji wake.
Ameeleza pia kuwa kupitia kamati hizi, Mamlaka imeweza kuboresha mahusiano na wananchi wanufaika wa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa uondoshaji majitaka wa Mbezi Beach ambao unaendelea kutekelezwa, mradi wa ujenzi wa vituo vya huduma kwa umma ambao umekamilika, miradi ya uondoshaji majitaka pembezoni mwa mji wa Dar es Salaam na miradi ya uondoshaji majitaka kwa mfumo rahisi yenye lengo la kuboresha kuepusha uchafuzi wa Mazingira na kuboresha afya za wananchi wake.
“Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupitia Mamlaka katika kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam na Pwani, hivyo nizipongeze kamati zote kwa ushiriki wenu mzuri kwenye zoezi hili na nizidi kuwatia moyo kuendelea na nguvu hiyo hiyo kwenye miradi inayoendelea kutekelezwa,” ameeleza Mhandisi Modesta.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Sinza ,Ndugu Raphael Awino ameipongeza Mamlaka kwa kazi kubwa inayoifanya ya kubuni na kutekeleza miradi yenye kukidhi mahitaji ya wananchi hususani miradi ya usafi wa mazingira.
“Hii ni miradi bora ambayo moja kwa moja inalenga kuokoa afya ya mwananchi mmoja mmoja kwa kuwa kero ya uchafuzi wa Mazingira kwenye maeneo yetu ilikuwa kubwa sana, hivyo mradi huu ni faraja sana kwetu,” ameeleza.
Pia amepongeza uwepo wa kamati hizi za kushughulikia malalamiko kwa kuwa zimesaidia sana katika kurahisisha utekelezaji wa mradi, pili mradi umeleta hamasa kwa wananchi kuupenda na kuwa na hamu nao na kuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika hatua zote za utekelezaji,” ameeleza Ndugu Msigani.
Nae mmoja wa wajumbe wa kamati ya kushughulikia malalamiko wa Kata ya Sinza, mtaa wa Sinza C Ndugu John Shija amesema kuwa kazi kubwa inayofanyika kwenye kamati ni kusikiliza malalamiko na maoni ya wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi na kutoa suluhu juu ya changamoto iliyowasilishwa ili mradi uendelee kutekelezwa.
Ameongeza kuwa kamati hizi zimesaidia sana kuimarisha uelewa wa wananchi kwenye miradi kwa kuwa wengi wao hawakuwa na malalamiko mengi zaidi ya kutaka sana ufahamu na maboresho zaidi.