Na: Rahma Khamis Maelezo 13/1/2024
Wakala wa vipimo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wametiliana saini hati ya makubaliano ya ushirikiano ili kuimarisha utendaji kazi wao.Â
Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini huo huko Ukumbi wa Dokt Mwinyi kituo cha maonesho ya biashara Nyamanzi Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara SMT Dkt. Hashil Abdalla amesema ni vyema kuimarisha mashirikiano kati ya taasisi hizo ili kuhakikisha vipimo vyote na thamani ya fedha inamfikia mtumiaji kwa usahihi.
Amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Wakala wa Vipimo ndio taasisi pekee inayopaswa kusimamia matumizi sahihi ya vipimo kwa kuhakikisha kuwa vipimo vinavyotumika katika biashara viko sahihi, na kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo ili kuepusha madhara yatokanayo na vipimo batili na kulinda walaji na watumiaji.
Aidha amesema makubaliano hayo yatasaidia kuimarisha utendaji wa kazi na kuongeza ufanisi utakaopelekea kufikia malengo ya Taasisi hizo.
Mkurugenzi wa wakala wa Vipimo Zanzibar ZAWEMA Mohammed Simai Mwalim ameeleza kuwa endapo vipimo vitasimamiwa kwa usahihi katika bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi itasaidia Serikali kukusanya kodi kwa usahihi.
Hata hivyo alisema endapo vipimo hivyo havitasimamiwa vyema itasababisha wananchi kupata kupata huduma au bidhaa ambazo haziendani na thamani ya fedha wanayotumia.
Mkurugenzi Mohammed alitoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara wote wa Tanzania bara na Zanzibar kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi na endapo watakutana na changamoto yoyote inayohusu vipimo wafike kwenye ofisi za Wakala wa Vipimo kwa ajili ya kupata msaada wa kitaalamu.
Hata hivyo aliwaonya Wamiliki wa vipimo kutochezea vipimo kwa lengo la kuwaibia wananchi, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kufanya vitendo hivyo ambavyo vinakatazwa hata kwenye maandiko matakatifu.
Nao Washiriki walioshuhudia utiaji wa saini huo walisema kuwa makubaliano hayo yametiwa saini katika kipindi muafaka cha kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na yataongeza mashirikiano zaidi ili kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi hayo.
Hati hiyo ya makubaliano ya kiutendaji yalisainiwa na Mtendaji Mkuu wakala wa vipimo Bara (WMA) Stela Kahwa na kwa upande wa Zanzibar Mkurugenzi wakala wa vipimo Zanzibar ZAWEMA Mohammed Mwalim Simai.