Home BUSINESS TUMIENI MAFUNZO HAYA KUPUNGUZA KERO KWA WAFANYABIASHARA- MHE. SERUKAMBA

TUMIENI MAFUNZO HAYA KUPUNGUZA KERO KWA WAFANYABIASHARA- MHE. SERUKAMBA

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, akizungumza katika hotuba yake yakumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Peter Serukamba, kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Biashara kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Rukwa, Simiyu, Katavi na Tanga yanayofanyika mkoani Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Peter Serukamba, akizungumza alipokuwa akidungua rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Biashara kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Rukwa, Simiyu, Katavi na Tanga yanayofanyika mkoani Singida.

SINGIDA 

Maafisa Biashara nchini, wametakiwa kutoa elimu kwa wananchi sambamba na kupunguza kero mbalimbali zinazojitokeza zikiwemo gharama zisizo halali za urasimishaji biashara suala ambalo Serikali imekuwa ikilipigia kelele mara kwa mara.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Peter Serukamba, ameyasema hayo tarehe 9 Januari, 2024 wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Biashara kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Rukwa, Simiyu, Katavi na Tanga yanayofanyika mkoani Singida.

“Mafunzo haya ni muhimu, ukizingatia kwamba hivi sasa masuala ya uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwemo utoaji wa huduma za Leseni za Biashara na Viwanda yanafanyika kwa njia ya mtandao kupitia Mifumo ya Kielektroniki au mifumo ya TEHAMA hivyo muwe sehemu ya kufanikisha haya,” amesema Mhe. Serukamba

Ameeleza kuwa ni matumaini yake kuwa, mafunzo haya yatakuwa chachu kwa maafisa biashara, ambayo yatawawezesha kuboresha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na wawekezaji. Pia, mafunzo haya ni nyenzo ya kupunguza kero na gharama za urasimishaji biashara, ikiwa ni utekelezaji wa uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini.

Ameongeza kuwa mpango huu wa mafunzo umezingatia umuhimu wa Maafisa Biashara kuwa karibu na wananchi, kwa kutoa huduma bora, saidizi na elimishi kwao ili kipato chao kikue na hatimaye Serikali ipate kodi na uchumi wa nchi uweze kuimarika.

Awali Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa huo kufungua mafunzo hayo, ameeleza kuwa, Maafisa Biashara wanatakiwa kubadilisha mtazamo na kutambua majukumu ya Idara na kada yao na kuachana na mtazamo wa kuwa wakusanya mapato pekee na kufunga biashara.

Amewataka kuwatambua wafanyabiashara katika maeneo yao na kusikiliza kero za wafanyabiashara zinazosababisha kufunga biashara na kuzitafutia majawabu ili biashara zao ziendelee kuwepo na kuimarika.

Aidha amewataka kutambua malengo ya idara yao ambayo ni mpya na majukumu yake, yakiwemo kuainisha fursa za uwekezaji na kuweka mazingira wezeshi kukuza biashara na kuinua uchumi wa Halmashari na mkoa husika.

“Kama mnavyofahamu, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara nchini, ili kuendana na azma ya kufanya mageuzi ya kiuchumi na viwanda kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu ya jamii, kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III),”amefafanua Bw. Nyaisa.

Mafunzo haya yaliyoandaliwa na BRELA kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Viwanda na Biashara, yana lengo la kuwajengea uwezo Maafisa Biashara wote nchini ambapo mafunzo haya endelevu, yameshafanyika kwa baadhi ya Maafisa Biashara katika mikoa yote ya Tanzania Bara na yataendelea kutolewa kwa Maafisa Biashara ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria mafunzo kama haya katika mikoa yote.

Previous articleSOMA HABARI KATIKA MAGAZETI YA LEO JANUARI 10-2024
Next articleWATU 3 WAFARIKI DUNIA KWA MAFURIKO MOROGORO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here