Tarehe 11 January , 2024
Msajili wa Hazina Tanzania Bara Bw. Nehemiah Kyando Mchechu, amefanya ziara ya kikazi visiwani Zanzibar kwa kumtembelea Msajili wa Hazina wa Zanzibar Bw. Waheed Muhammad Ibrahim Sanya. Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa Memorandum of Understanding iliyotiwa saini mwezi April, 2023 kati ya ofisi hizo mbili. Makubaliano hayo yana lengo la kuijengea uwezo Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar katika kusimamia Mashirika ya Umma kwa kutumia uzoefu wa muda mrefu wa ofisi ya msajili wa Hazina Tanzania Bara. Ofisi ya Msajili bara ilianzishwa mwaka 1959 ambapo mpaka sasa ina mashirika zaidi ya 300 katika sekta mbalimbali za kibiashara na zile huduma. Ofisi ya Msajili Zanzibar kwa sasa inasimamia mashirika yapatayo 17 na ilianzishwa mwaka 2021 na imejipanga kuhakikisha mashirika hayo yanaleta tija kulingana na malengo ya kukuza uchumi kulingana na maono ya Mheshimiwa Daktari Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar. Itakumbukwa kwamba, rai na msukumo wa kuyafanya Mashirika ya Umma yanachochea uchumi yamekuwa kipaumbele ya Serikali zote mbili.
Katika mazungumzo yao, wasajili wamekubaliana
1. Kuongeza weledi katika kusimamia mashirika kwa manufaa ya umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Kubadilishana wafanyakazi na uzoefu wa utendaji wa kazi kitaalam.
3. Kuwa kioo cha ufanisi wa utendaji kazi na kushiriki kikamilifu katika kudumisha Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Pamoja na ziara ya kikazi, Bw. Mchechu pia yupo visiwani Zanzibar kushiriki katika maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
MWISHO