Home BUSINESS MAAFISA BIASHARA WATAKIWA KULETA MABADILIKO KATIKA IDARA

MAAFISA BIASHARA WATAKIWA KULETA MABADILIKO KATIKA IDARA

SONGIDA

Maafisa Biashara wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kubadilisha mitizamo yao na kutekeleza majukumu ya idara yao mpya ya Biashara Viwanda na Uwekezaji kwa ufanisi.

Hayo yameelezwa leo tarehe 12 Januari, 2024 na Mkurugenzi wa Leseni wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Andrew Mkapa, wakati akifunga mafunzo ya Maafisa Biashara kuhusu Sheria ya Leseni za Biashara na Viwanda, yaliyofanyika kwa siku nne mkoani Singida.

“Ndugu washiriki, mafunzo haya yasiishie hapa, tuendelee kuwasiliana hata tukirudi katika maeneo yetu ya kazi, tushauriane pale inapohitajika na tubadilishane uzoefu juu ya jambo lolote,” amesema Bw. Mkapa

Akitoa ushauri kwa maafisa biashara hao Bw. Mkapa ameeleza kuwa baada ya mafunzo hayo endapo kutakuwa na ulazima wa kuwa na mabadiliko katika utendaji kazi ni vyema busara ikatawala zaidi katika kuwasilisha namna ya kuleta mabadiliko hayo katika utekelezaji wa majukumu.

Akitoa shukrani baada ya mafunzo hayo, Afisa Biashara wa Manispaa ya Mpanda Bw. Paul Kahoya, ameahidi kwenda kuyatekeleza yote waliyojifunza sambamba na kuzisoma Sheria ambazo zitakuwa muongozo katika kutekeleza majukumu yao.

Aidha ameongeza kuwa yote waliyoyapata ni nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu yao na hivi sasa wamepewa idara, hivyo anaamini kwamba uanzishwaji wa idara hiyo ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara itawawezesha wao kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuwa ni wazi kwamba Serikali imeona kwamba kuna tija, hivyo watafanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria na miongozo waliyopewa.

Mafunzo hayo kwa Maafisa Biashara kutoka mikoa ya SIngida,Dodoma, Rukwa, Simiyu, Katavi na Tanga yaliandaliwa na BRELA kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Viwanda na Biashara, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here