Home BUSINESS LATRA YAIFUNGULIA KAMPUNI YA KILIMANJARO

LATRA YAIFUNGULIA KAMPUNI YA KILIMANJARO

Mwandishi wetu

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeruhusu Kampuni ya Kilimanjaro Truck Company Limited kuendelea kutumia rasmi leseni na ratiba za mabasi yake 35 baada ya kutekeleza masharti iliyopewa.

Hatua hiyo inakuja baada ya Kampuni hiyo kusitishiwa leseni Januari sita mwaka huu na LATRA baada ya kukiuka masharti ya leseni ya mtoa huduma kwa kutoa huduma bila kutumia mfumo wa tiketi mtandao na kutoza nauli zaidi ya viwango vilivyoidhinishwa na Mamlaka husika.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Jijini Dar es salaam Leo Januari 14, 2024 Mkurugenzi Mkuu LATRA, Habibu Suluo amesema mabasi hayo yataanza kufanya kazi kuanzia Leo baada ya kukamilisha masharti iliyopewa.

Amesema LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kikosi Cha Usalama Barabarani pamoja na kituo Cha Taifa Cha kuhifadhi kumbukumbu (NIDC) imehakiki mfumo wa tiketi mtandao wa Kilimanjaro Truck Company Limited .

Amesema kabla ya kuruhusiwa Kampuni hiyo ilitakiwa kutekeleza masharti iliyopewa ikiwemo kutumia mfumo wa tiketi mtandao, kuzingatia viwango vya ukomo wa nauli vilivyowekwa na LATRA .

Mbali na mfumo huo pia ilipaswa kuwasilisha maombi ya kurejesha huduma ambayo itaiwezesha LATRA kuhakiki mfumo wa tiketi mtandao, nauli zilizoigizwa kwenye mfumo na madaraja ya mabasi hayo 35 kabla ya kuruhusu leseni na ratiba za mabasi husika kuendelea kutumika.

“LATRA inapenda kutoa taarifa kuwa imeruhusu leseni na ratiba za mabasi 35 ya Kilimanjaro Truck Company Limited kuanza kutumika kuanzia Leo Januari 14 hii ni baada ya kutimiza masharti “amesema Suluo.

Aidha aliwataka watoa huduma wote kufanya kazi Kwa mujibu wa sheria ili kuepuka kuchukukuliwa hatua mbalimbali.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Kampuni hiyo Dickson Ngowi aliishukuru LATRA Kwa ushirikiano iliotoa pindi Kampuni hiyo ilivyositishiwa leseni na kuhaidi masharti yote waliyopewa wataendelea kuyatekeleza.

“Magari yetu yote yamekaguliwa na yamepewa stia maalumu ambapo mlangoni kabisa yamebandikwa daraja husika la gari ili kumsaidia abiraia kujua anapanda gari la daraja gani”amesema Ngowi.

Naye Mratibu mwandamizi wa Polisi Salumu Morimori aliwaomba watoa huduma kuzingatia sheria za Mamlaka husika ikiwemo kutii sheria.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here