Na: Eleuteri Mangi, WANMM
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na utekezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Najma Murtaza Giga Januari 24, 2024 jijini Dodoma wakati wa kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ambao ulisainiwa 2022 na umeanza kutekelezwa 2023 na unatarajiwa kukamilika 2027.
“Tumeridhishwa na utendaji kazi wa Wizara, tuendelee kushirikiana na kamati hii katika kazi mnazofanya ili mnayopanga kuyatekeleza yaendelee na tufanye kazi kwa pamoja” amesema Mhe. Najma.
Akifafanua na kujibu hoja za Wabunge wakati wa kujadili taarifa hiyo mbele ya kwa kamati hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mkazi Mhe. Jerry Silaa amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ardhi ili wapate haki zao stahiki kwa wakati.
Waziri Silaa ameongeza kuwa Wizara hiyo imejipanga kuwahudumia Watanzania kupitia mfumo wa TEHAMA ambao utarahisisha kuwahudumia wananchi wengi na utasidia kupokea na kutatua malalamiko yanayotolewa na wananchi hatua itakayosaidia kuwapatia haki zao kwa wakati.
Aidha, Waziri Silaa amesema kuwa wamezipokea pongezi zilizotolewa na Wajumbe hao wa Kamati kwa kuwa zinawatia moyo na kuwaongezea kasi ya kuwahudumia wananchi ili wapate haki zao kwa wakati.