DAR ES SALAAM
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk.Ashatu Kijaji, amesema Bdhaa zinazozalishwa katika viwanda vya Tanzania zina ubora wa kukidhi katika soko la Afrika na Dunia.
Dk. Kijaji amebainisha hayo leo Januari 4, 2024 katika ziara yake ya kutembelea kiwanda cha Multi Cable Limited (MCL) kinachozalisha vifaa vya umeme kilichopo Chang’ombe, Jijini Dar es Salaam.
Lengo la ziara hiyo ni kuona kinachozalishwa katika viwandani vya ndani mazingira ya watumishi wanofanya kazi huko ili kuweza kuboresha.
Amesema kutokana na kile alichokiona katika kiwanda hicho na bidhaa zinazozalishwa kuwa na nembo ya TBS ya Tanzania, ni muda wa wazalishaji wa ndani kuingia kwenye soko la eneo huru la Afrika.
“Tanzania ipo katika masoko ya kikanda, Afrika Mashariki na nchi za Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, hivyo tunahakikisha bidhaa zetu zinafika katika masoko hayo.
“Leo hii nimewaelekeza wenye kiwanda hiki, tunapomaliza ziara hii, twende ofisini tukutane ili tuweze kuwaelekeza tunaingiaje kwenye Soko la Eneo Huru la Afrika,” amesema Dk. Kijaji.
Aidha ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi na maslahi ya wafanyakazi wao. Afrika.
Kwa upande wake Mwanasheria wa kampuni ya MCL, Kassmary Ahmed, amesema wanatengeneza vifaa vyote vya umeme ikiwamo Transifoma, Mita na nyaya tangu mwaka 2002.
Amesema wamefurahia ujio wa waziri wa viwanda kwani lengo lao ni kuongeza ajira kwa vijana na kuinua uchumi wa Taifa.
“Tunaungana na wizara katika kukuza, uboreshaji na kuongeza ubora wa bidhaa wanazozalisha. Kampuni hii pia inajihusisha na masuala ya kijamii.
Amesema changamoto inayowakabili ni umeme kwani inawafanya wateja wasipate bidhaa kwa wakati.