TMDA
Home Uncategorized SERIKALI YAFANYA MABADILIKO YA UONGOZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA TANGA-BOMBO

SERIKALI YAFANYA MABADILIKO YA UONGOZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA TANGA-BOMBO

Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya mabadiliko ya kiuongozi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo ikiwa na lengo la kuhakikisha inaendelea kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma bora za Afya kwa Watanzania.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali Watu Wizara ya Afya Bw. Daniel Temba wakati wa halfa ya makabidhiano ya ofisi kwa Mganga Mfawidhi Mpya Dkt. Frank Shega kutoka kwa aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dkt. Naima Yusuf katika Hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Japhet Simeo.

Alisema Serikali inayoongozwa na Rais. Dkt. Samia Suluhu kwa kipindi cha muda mfupi imefanya maboresho makubwa sana kwenye sekta ya Afya katika maeneo ya miundombinu,vifaa tiba na watumishi, Hivyo mabadiliko ya Uongozi huo unalenga kuzidi kuleta mapinduzi kwenye utoaji wa huduma bora kwa wananchi .

“Kutokana na maboresho yaliyofanywa na Mhe. Rais. Dkt. Samia katika sekta ya Afya, Watumishi wote tunadeni la kutimiza wajibu wetu wa kuhakikisha tunawapatia wananchi huduma bora za Afya pia kupitia mabadiliko haya ya uongozi tunategemea kila mmoja wetu ashirikiane na uongozi wa ndani na nje ya Wizara kuhakikisha wanatoa huduma nzuri na bora kwa watanzania kwa kuwa utaalamu wetu unategemewa sana na wananchi. ” Alisema Bw. Temba.

Aidha, aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Tanga na viongozi wa CCM Mkoa kwa kuwa wamekuwa jicho la kuangalia mahitaji ya wananchi yaweze kufikiwa kwa ubora unaotakiwa.

Awali akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ofisi hiyo Mganga Mfawidhi mpya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo Dkt. Frank Shega aliomba ushirikiano kwa sababu wanakwenda kufungua ukurasa mwingine wa kiutendaji wenye lengo la kuboresha huduma na kuzitaka Timu ya Viongozi wa Hospitali (RRHMT) na Timu ya Uongozi wa Afya Mkoa (RHMT) kushirikiana ili kwa pamoja kuweza kufikia malengo yaliyowekwa kwa wakati.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Japhet Simeo alisema Dkt. Naima anayemaliza muda wake amefanya kazi kubwa sana kwa kujitahidi kubuni vitu mbalimbali ili kuhakikisha wanaongeza mapato kwenye Hospitali hiyo.

    

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Open chat
GREEN WAVES MEDIA
Ahsante kwa kutembeiea SERIKALI YAFANYA MABADILIKO YA UONGOZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA TANGA-BOMBO