Home BUSINESS ZAIDI YA ASILIMIA 99 YA WAGUSWA WA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA...

ZAIDI YA ASILIMIA 99 YA WAGUSWA WA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA (EACOP) WALIPWA FIDIA

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umefanikiwa kuwalipa fidia kwa asilimia 99.8 kwa watu wote walioguswa na mradi pamoja na kuhakikisha unaendelea kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi na kibiashara kwa watanzania ikiwemo ujenzi pamoja na ajira kwa wanakijiji katika Mikoa nane ambapo mradi unatekelezwa.

Akizunguza leo Desemba 22, 2023 Jijini Dar es Salaam na Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu Maendeleo ya Mradi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki upande wa Tanzania (EACOP), Bi. Catherine Mbatia, amesema kuwa utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri na mpaka sasa tayari wamelipa fidia asilimia 99.8 kwa watu wote walioguswa na mradi.

Bi. Catherine amesema kuwa utekelezaji wa mradi unaendelea, huku watanzania kutoka maeneo tofauti ikiwemo ambao wameguswa na mradi kwa kuchukuliwa nyumba zao pamoja mashamba (ardhi).

“Tumewalipa fidia watu wote ambao ardhi yao imeguswa na mradi pamoja na wale ambao wamelazimika kuhama ambapo tumewajengea nyumba za kisasa tofauti na zile walizokuwa wanaishi awali” amesema Bi Catherine.

Amesema kuwa wameweza kujenga Nyumba za kisasa 339 kwa ajili ya kuwapatia wanakijiji ambao wamepisha utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi.

Bi. Catherine amebainisha kuwa Desemba, 2023 wamepokea mabomba yenye urefu wa kilometa 100 kutoka nchini China kwa ajili utekelezaji wa mradi bomba la mafuta ghafi, huku akieleza kuwa mpaka sasa wameweza kutumia Dola za Marekani 141 kwa ajili ya kununua vifaa nchini Tanzania.

Afisa habari wa EACOP Bw. Abass Abraham, amesema kuwa upana wa bomba la mafuta ghafi lina ukubwa wa kipenyo cha setimita 24 ambapo wataweza kutumia eneo lenye upana wa mita 30.

“Bomba la mafuta ghafi litafukiwa chini ya ardhi na juu mazingira yatakuwa katika hali ya kawaida na utekelezaji wa ujenzi umezingatia viwango vya kimataifa hivyo hakutakuwa na uharibifu wowote ikiwemo viumbe vya baharini” amesema Bw. Abraham.

Bw. Abraham amesema kuwa katika utekelezaji wa mradi wa EACOP Kampuni ya Total Energy ya Ufaransa ambayo imegundua uwepo mafuta nchini Uganda imewekeza asilimia 62, huku kampuni ya CNOOC kutoka China imewekeza asilimia nane (8).

Amesema kuwa serikali ya Tanzania na Uganda imewekeza asilimia 15 kila mmoja kwa ajili ya kufanikisha uwekezaji wa mradi wa EACOP.

“Katika utekelezaji wa mradi huu kutakuwa kambi 16 ambapo kambi 4 zitakuwa Uganda na kambi 12 zitakuwa Tanzania, pia kutakuwa na pampu mbili katika nchi hizo mbili” amesema Bw. Abraham.

Mkuu wa Idara ya Ushirikishwaji Jamii Mradi wa EACOP, Bi. Fatuma Msumi, amesema kuwa kuna vijiji 233 ambapo mradi umepita na kila hatua wamekuwa wakipewa taarifa ili kujua nini kinachoendelea.

Bi. Msumi amesema wamekuwa na utaratibu wa kuitisha mikutano na makundi tofauti ikiwemo wanawake, wanaume pamoja na vijana ili kueleza changamoto gani ambazo zipo katika utekelezaji wa mradi na kuangalia nmana ya zitatua.

Amesema kuwa wamefanikiwa kufanya mikutano 3,900 katika maeneo mbalimbali pamoja na kupelekea ripoti kwa Wakuu wa Wilaya na Mkoa ambapo mradi huo umepita.

Mradi wa bomba la mafuta ghafi linapita katika mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Mradi huo una urefu wa jumla ya kilomita 1443 kwa upande wa Tanzania na kilomita 266 zipo nchini Uganda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here