Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Ndugu Elibariki Naman mkazi wa Jorodom, Katesh ambaye ni muathirika wa Mafuriko yaliyotokea Wilayani Hanang. Ndugu Elibariki alikuwa akielezea jinsi majirani zake walivyopoteza maisha pamoja na makazi yao katika maafa hayo.
Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan December 07,2023 ametembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko katika Mji wa Katesh Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara na kuongea na Wananchi wa Katesh ambapo amewapa pole na kuwatia moyo kuwa msiba uliotokea ni wa Taifa na sio wa Manyara pekee yao huku akiwahakikishia kuwa Serikali ipo pamoja nao. –
Rais Samia amesema “Ni kazi ya Mungu na hatujui Mungu katuletea hili kwa makusudi gani, kwetu sisi ni kupokea na kumshukuru hatuwezi kumlaumu na hili sio letu pekee yetu mwaka jana au mwaka juzi lilitokea Malawi tukaenda kuwasaidia nimekwenda hali ni kama hii utafikiri hakukuwa na nyumba kabisa na ni eneo kubwa, ni kushukuru na kuchukua tahadhari, sasa maeneo ya maji tuyapishe maji yachukue nafasi yake sisi tukae pembeni”
“Poleni sana kwa tukio, nimeona nije nione mwenyewe toka juzi mambo yametokea nilikuwa safari mlisikia lakini Waziri Mkuu mara moja na Serikali yote ilikuwa hapa nikawapa maelekezo nini cha kufanya wamejitahidi sana kwahiyo leo nimerudi nikaona nije mwenyewe”
“Haya ni matendo ya Mungu kwetu sisi ni kupokea na kushukuru, ingekuwa kuna Mtu kule kafungulia maji tungesema huyu Mtu huyu lakini ni Mungu mamvua yamenyesha huko yameporomosha yametokea yaliyotokea, poleni sana tupokee ni msiba wa Taifa wala sio wenu pekee yenu ni wetu sote Taifa”
“Nchi nyingine Marafiki zetu wanatoa pole sana kwa hili lililotupata, nataka niwaambie, Serikali tupo pamoja nanyi bado Mawaziri vyombo vya ulinzi na wengine wote wako hapa, tunaangalia hali halisi jinsi ya kusaidia, tunaangalia jinsi ya kuepusha Wananchi kuingie tena kwenye balaa kama hili, poleni sana Serikali tupo nanyi”
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa eneo la Jorodom ambalo limeathirika na Mafuriko pamoja na maporomoko ya matope na mawe Wilayani Hanang Mkoani Manyara tarehe 7 Desemba, 2023. Rais Samia alijionea uharibifu mkubwa uliotokea na kuwapa pole Waathirika wa maafa hayo na kuwaeleza kuwa Serikali ipo pamoja nao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga akielezea kuhusiana na athari za mafuriko yaliyotokea katika eneo la Jorodom Katesh Wilayani Hanang. Rais Samia ametembelea eneo hilo Mkoani Manyara tarehe 7 Desemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimfariji muathirika wa mafuriko yaliyotokea Katesh Bi. Salome Elifuraha ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tumaini iliyopo Katesh, Hanang. Mama amepoteza watoto wawili kwenye maafa hayo huku mtoto wa tatu akiwa bado hajapatikana hadi sasa. Rais Samia aliwatembelea majeruhi wa maafa ya mafuriko hayo ambao wamelazwa katika hospitali hiyo ya Wilaya Mkoani Manyara tarehe 7 Desemba, 2023.