Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga (katikati), akimsikiliza Mkandarasi wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Miradi ambayo inafanyika kwa ajili ya kuboresha Miundombinu ya umeme katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Ilala tarehe 1 Desemba, 2023 Jijini Dar Es Salaam.
Dar Es Salaam
Serikali imeilekeza Idara ya Usambazaji wa Umeme ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuchukua hatua kwa yeyote atakayehusika na kuwapa kazi na mikataba Wakandarasi wa Usambazaji wa vifaa vya umeme ambao hawana uwezo wa kufanya kazi hiyo ama wanaofanya kazi kwa uzembe.
Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema hayo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Miradi ambayo inafanyika kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umeme katika Kituo cha Kupoza umeme cha Ilala tarehe 1 Desemba, 2023 Jijini Dar Es Salaam.
Amesema Idara hiyo iwasimamie wakandarasi waliopewa mikataba ya kazi ya kusambaza vifaa kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye njia za kusambaza umeme ambazo zinapeleka umeme kwa wananchi ili vifaa hivyo vipatikane kwa wakati kwa kuwa upatikaji wake umekuwa unasumbua.
Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga (katikati), akimsikiliza Mkandarasi wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Miradi ambayo inafanyika kwa ajili ya kuboresha Miundombinu ya umeme katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Ilala tarehe 1 Desemba, 2023 Jijini Dar Es Salaam.
“Kwa hiyo kama unafanya uzembe kwa kuwapa kazi na mikataba wasambazaji ambao hawana uwezo au wanaoshindwa kufanya kazi na hamuwachukulii hatua tutaanza na anayehusika, pamoja na hao wakandarasi kwa sababu tumewaelekeza maeneo hayo ni mjini ni lazima wananchi hao wapate umeme wa uhakika”, alisisitiza Mhe. Kapinga.
Sambamba na hilo ameagiza Idara ya Usambazaji kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kama mkandarasi aliyepewa kazi hatekelezi kwa wakati majukumu yake na kufanya kazi kwa uzembe asiongezewe mkataba wake pale utakapokwisha badala yake wawapatie kazi wakandarasi wenye uwezo wa kutekeleza kazi zao kwa wakati ikiwa ni pamoja na kupeleka vifaa vinavyohitajika kama Nguzo, Mashineumba, Waya na vifaa vingine muhimu katika maeneo husika.
“Serikali inatoa fedha vyingi za kutekeleza miradi, kwa hiyo hatutaweza kuvumilia wala kuona njia za kupeleka umeme kwa wananchi haziboreshwi kwa sababu ya uzembe wa watu wachache, kuna laini za umeme ambazo zinasumbua sana ikiwa ni pamoja na kukatikatika sana kwa umeme Mbagala, Kurasini na Kigamboni niwakikishie wananchi wa maeneo haya kuwa Serikali inafanya kila linaloliweza kuboresha hali ya upoatikanaji wa umeme katika maeneo hayo”, alisema Mhe. Kapinga.
Amesema wananchi wamekuwa na malalamiko ya kukatika kwa umeme, pamoja na changamoto iliyopo sasa, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya umeme ili kuhakikisha kuwa itakapotengemaa wananchi wanapata huduma ya uhakika.
Kwa sababu hata tukiwa na umeme wa uhakika kama hatujaboresha miundombinu ya umeme hasa njia za kusambaza umeme kwa wananchi bado kutakuwa na changamoto kubwa,
Kituo hicho cha Ilala kitaboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Ilala, Kigamboni, Kurasini na Temeke.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kapinga, amefanya ziara katika kituo cha kupoza umeme cha Mbagala na kuwaagiza TANESCO kuwashirikisha Viongozi wa Chama, Serikali za Mitaa na Wilaya kwa kila hatua ya miradi inayoendelea katika maeneo yao ili waweze kuwaeleza wananchi wanaowazunguka.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda ambaye aliambatana na Naibu Waziri huyo ameunga mkono kauli hiyo kwa kusema kuwa wao ndiyo Viongozi wanaokutana na wananchi kila siku hivyo ni vyema wakapatiwa taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo mapema wawafikishie wananchi ili hata TANESCO watakapoeleza changamoto inayowakabili wananchi hao waipokee kwa mwitikio chanya.