Home LOCAL LETENI ANDIKO LA MFUMO WA KADA YA USTAWI WA JAMII KUFANYA KAZI...

LETENI ANDIKO LA MFUMO WA KADA YA USTAWI WA JAMII KUFANYA KAZI KWA TIJA ZAIDI: WAZIRI MKUU MHE. KASSIM MAJALIWA

 

Na WMJJWM, Dar es Salaam

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, kuandaa andiko litakalowezesha kada ya Ustawi wa Jamii kusimama imara zaidi na kufanya kazi kwa tija zaidi baada ya kuundwa kwa wizara rasmi ya ambayo ni mama kwa kada hii tofauti na kabla ya kutenganishwa toka Idara kuu ya afya.

Akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii na Wiki ya Ustawi wa Jamii Desemba, 18, 2023 jijini Dar es Salaam, Mhe. Majaliwa amesema kwa muda sasa kumekuwa na changamoto ya kushughulikia masuala ya Ustawi wa Jamii na jamii kwa jumla kutokana na Wataalamu wa ustawi wa Jamii kuwa chini ya usimamizi wa Waganga wakuu wa Mikoa.

“Serikali imekuwa ikiajiri Maafisa Ustawi wa Jamii lakini changamoto wanayoipata ni usimamizi na hili mmelisema hapa, hivyo nakuagiza Mhe. Waziri pamoja na Wataalam wako mkaandae andiko la kitaalam kisha mliwasilishe kwenye ofisi yangu ili tuweze kumshauri Mhe. Rais, Ili kuongeza tija” amesema Majaliwa.

Wakati huo huo Waziri Mkuu Majaliwa, ameitaka Jamii kuhakikisha suala la Maadili linapewa nguvu na Jamii nzima na kuwa mstari wa mbele kwenye kukemea na kufichua viashiria vya vitendo vya kikatili ndani ya jamii kabla ya madhara kutokea huku akipongeza Wizara kwa kushirikiana na TCRA kwa kuja na mpango wa vipindi vya redio vitakavyorushwa kwenye redio zaidi ya 150 kote nchini na kuangazi masuala ya maadili.

Kuhusiana Miaka 50 ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Mhe. Majaliwa ameitaka taasisi hiyo kuendelea kuboresha Mitaala yake ili iweze kuendana na mazingira ya sasa, huku akiitaka Wizara kuwatumia wataalam waliofanikisha bunifu mbalimbali ziweze kuwa msaada kwa jamii hususan Program Tumizi ya ‘Social Protections.’

Akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha ajira 350 zilizowezesha kuongeza wigo wa utoaji wa huduma.

Dkt. Gwajima amesema, kwa sasa uelewa wa wananchi kuhusu huduma za Ustawi wa Jamii umeongezeka ambapo kwenye Wiki ya Ustawi wa Jamii jumla ya watu 7,766 walipatiwa huduma mbalimbali ikiwemo, Msaada wa Kisaikolojia, Afya ya Akili na Utatuzi wa Migogoro ya Ndoa.

“Shabaha yetu ni kuona kila palipo na shughuli za kijamii anakuwepo Afisa Ustawi, hii itasaidia huduma hizi kueleweka lakini pia kupunguza masuala ya ukatili,” amesema Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amesema Wizara yake kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeandaa vipindi vya Redio 22 vitakavyorushwa kwenye kupitia Redio 150 kote nchini kwa ajili yakutoa elimu ya madili na kupinga ukatili na ameonya wazazi na walezi kuacha watoto kulelewa na mitandao ya kijamii kwani athari zilizopo ni kubwa.

Akizungumza wakati wa kilele hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatuma Toufiq, amesema Kamati yake itaendelea kuishauri Serikali ili Maafisa Ustawi waweze kuajiriwa wa kutosha.

MWISHO

Previous articleWANANCHI KYELA WATAKIWA KULIMA KILIMO CHA KAKAO KIBIASHARA
Next articleBRELA ANA KWA ANA NA WAFANYABIASHARA MBEYA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here